Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya ya mkinga, amchefua waziri mkuu…aagiza achunguzwe

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bibi
Judica Omari achunguze utendaji kazi wa Mweka Hazina wa Halmashauri ya
wilaya ya Mkinga, Bibi  Juan Mening.


Amesema
hajaridhishwa na utendaji wake kwa kuwa ameshindwa kusimamia ukusanyaji
wa mapato na hata hicho kidogo kinachokusanywa hakifikishwi Serikali.

Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akizungumza
na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga pamoja na wananchi baada
ya kufungua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga akiwa katika
ziara  ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema
Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya
kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia
watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu  na haitosita kuwachukulia
hatua.

“Watumishi
fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya
vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo
wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”

Waziri
Mkuu aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa
kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma na pia watambue dhamana
kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa
aina yoyote.

Pia,
Waziri Mkuu amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga
kuhakikisha wanakuwa wakali katika usimamizi wa makusanyo ya mapato
pamoja na matumizi yake.

Wakati
huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku 18 kuaznia leo Jumatatu, Machi 2, 2020
kwa watumishi wa halmashauri hiyo wanaoishi jijini Tanga wawe wamehamia
katika kituo chao cha kazi na watakaoshindwa wabaki huko huko waliko.

Amesema
Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo
vyao vya kazi. “Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini
Tanga wawe wamehamia hapa ifikapo Machi 20 mwaka huu na wasiohamia
waendelee kubaki huko huko.”

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *