Mwenge wa uhuru tayari umewasili katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo Ijumaa Julai 28,2023 ambapo umepokelewa katika kijiji na kata ya Kolandoto ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Mapokezi ya Mwenge wa uhuru yamehudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa chama cha mapinduzi CCM, wadau mbalimbali pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo miradi kumi ya maendeleo itazinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi na Mwenge wa uhuru.
Aidha Mwenge wa uhuru katika Mkoa wa Shinyanga utakimbizwa umbali wa kilomita 571.5 na kuona, kuweka mawe ya msingi, kufungua na kuzindua jumla ya miradi 41 yenye thamani ya shilingi bilioni 14.27.
Miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 7.8 itawekewa mawe ya msingi, miradi 14 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.3 itazinduliwa, miradi 4 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 itafunguliwa huku miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni bilioni 1.5 itaonwa.
Mwenge wa uhuru unaongozwa na Bwana Abdalla Shaim Kaimu, kitaifa ulizinduliwa April mosi 2023 ambao mpaka sasa umekimbizwa katika mikoa 20 na kwamba katika Mkoa wa Shinyanga utakimbizwa katika Halmashauri zote sita.
Kauli mbiu ya mbio za mwenge kwa Mwaka huu inasema tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa.
Mkesha wa Mwenge wa uhuru leo utafanyika katika uwanja wa Saba saba Kambarage mjini Shinyanga.