Nacte yatangaza awamu ya nne ya udahili katika ngazi ya astashahada na stashahada kwenye vyuo na taasisi mbali mbali kwa mwaka wa masomo 2019/2020

Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linautangazia umma kwamba
limefungua dirisha la udahili kwa AWAMU YA NNE na ya mwisho, kwenye Vyuo
na Taasisi zinazotoa programu za Astashahada na Stashahada hapa nchini,
zinazotambuliwa na Baraza kuanzia tarehe  1 Novemba, 2019  hadi tarehe
10 Novemba, 2019 ambapo dirisha hilo litafungwa.


Hatua
hiyo imekuja kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Vyuo na Taasisi
mbalimbali kutaka nafasi zilizo wazi ziweze kujazwa. Kwa kuzingatia
hilo, Baraza linatoa wito kwa wahitimu wa Kidato cha Nne na Kidato cha
Sita na wale wote walio na nia na sifa za kujiunga na programu
mbalimbali kutumia fursa hii kutuma maombi ya udahili kwenye Taasisi na
Vyuo ambavyo bado vinapokea maombi ya udahili katika ngazi ya
Astashahada na Stashahada.

Aidha,
Vyuo na Tasisisi zitakazohusika kwenye awamu hii, zinaarifiwa kwamba
mfumo utakuwa wazi kupokea majina ya wanaodahiliwa ili kufanyiwa uhakiki
hadi hiyo tarehe 10 Novemba, 2019. 

Vyuo
na Taasisi zinazotaka kubadilisha taarifa za wanafunzi waliowasilishwa
na kuonekana kuwa na mapungufu yaliyopelekea kukosa sifa, nazo
zinashauriwa kufanya hivyo ndani ya kipindi hicho kuanzia leo tarehe 01
hadi 10 Novemba, 2019.

Ikumbukwe,
kwamba uhakiki wa majina yote yatakayowasilishwa utafanyika kuanzia
tarehe 11 hadi 15 Novemba, 2019, na  matokeo ya uhakiki yatatolewa
tarehe 17 Novemba, 2019.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)