NEMC YAUNGANA NA RAIS DKT SAMIA NISHATI SAFI, YATOA MSAADA WA MAJIKO S/MSINGI ARUSHA SCHOOL

Na Seif Mangwangi, Arusha

KATIKA kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi, Baraza la Taifa la hifadhi ya mazingira (NEMC), limetoa msaada wa majiko manne ya nishati safi ya kupikia (Gas stoves), kwa shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza (Arusha School).

Akizungumza wakati wa kukabidhi majiko hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Lilian Mkambuzi ambaye ni Afisa ukaguzi tathmini na majanga kwa jamii amesema msaada huo ni katika kuhamasisha jamii kutumia nishati safi na kuunga mkono juhudi za Rais Samia.

Amesema shule ya msingi Arusha yenye takribani wanafunzi 1600 imekuwa ikitumia kuni kama nishati ya kupikia chakula wanafunzi tangu mwaka 1934 ilipoanzishwa jambo ambalo limekuwa likichangia kuharibu mazingira kwa sehemu kubwa.

Lilian amesema NEMC baada ya kupata historia ya shule hiyo iliamua kutumia maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani kutoa msaada wa majiko hayo yenye uwezo wa kupika chakula chenye ujazo wa lita 700 kwa wakati mmoja.

“Katika majiko haya, majiko matatu yana ujazo wa lita 200 kila moja yenye gharama ya TZS 2400,000 kwa kila moja na jiko moja lina uwezo wa lita 100 lenye gharama ya TZS 1600,00…Gharama ya jumla kwa majiko na gesi ni taribani shilingi Milioni kumi (10,000,000),”amesema.

Amesema mbali ya zoezi hilo kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kama kinara wa nisahti safi ya kupikia barani Afrika, pia ni katika kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa mwaka 2024 unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wae wanatumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, afya ya jamii na kuboresha maisha.

“Matumizi ya mkaa na kuni yanachangia uharibifu wa mazingira kutokana ukataji miti, kuathiri afya ya jamii kutokana na moshi haswa wanawake na watoto ambao hutumia muda mwingi jikoni na pia kupelekea kuongezeka athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Arusha, Hashim Njau amesema matumizi ya kuni yamekuwa yakiwafanya kutumia gharama kubwa ambapo kila baada ya miezi miwili mkandarasi alilazimika kununua gari la kuni hivyo wanaishuruku NEMC kwa msaada huo.

Amesema majiko hayo yatasaidia wapishi kukamilisha majukumu yao kwa wakati na ufanisi zaidi na kuboresha afya na ustawi wa wanafunzi na taifa kwa ujumla.