Ni haki ya mwanahabari kupewa habari na taasisi zote za umma na sio hisani- mwakyembe

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo imezitaka ofisi za Umma kutoa taarifa kwa wanahabari kwa kuwa
siyo hisani na siyo hiyari, bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 (d).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe akizungumza na uongozi wa Arusha Press Club kuhusu namna bora
ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Habari, leo
Jijini Dodoma


Kauli hiyo
imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya tasnia ya Habari Dkt. Harrison
Mwakyembe alipokutana na ujumbe wa viongozi wa Chama cha Waandishi wa
Habari mkoani Arusha (APC), kupitia mradi unaouendesha wa Alternative Media leo jijini Dodoma.

“Serikali haina ugomvi na vyombo vya
habari, bila vyombo vya habari hatutaweza kuwahabarisha wananachi
masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu” amesema Dkt. Mwakyembe.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan
Abbasi (kushoto) akizungumza katika kikao cha Waziri wa Wizara hiyo Dkt.
Harrison Mwakyembe pamoja na uongozi wa Arusha Press Club kuhusu namna
bora ya kutekeleza majukumu yao ya kutoa habari sahihi kwa wananchi leo
Jijini Dodoma.

Aidha, amewakumbusha wanahabari kuwa kazi
wanayofanya ni muhimu sana ambapo nchi zilizoendelea bado wanatumia
vyombo vyao vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)
ambalo lina miaka zaidi ya 90 na linatangaza habari zake kwa lugha zaidi
ya 40 ili kuwafikia wananchi wake na dunia kwa ujumla.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha
Waandishi wa Habari kutoka mkoa wa Arusha Bw. Claud Gwandu amemshukuru
Waziri Dkt. Mwakyembe kwa mapokezi, majadiliano yenye tija kwa uwazi na
ukweli na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika sekta
anazozisimamia.
Mwenyekiti wa Arusha Press Club Bw. Claud Gwandu akizungumza jambo
wakati wa kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) ambapo walijadiliana masuala mbalimbali
yanaohusu tasnia ya habari leo Jijini Dodoma


“Tunamshukuru Waziri kwa kutupa nafasi
ili tuweze kushirikiana katika kuimarisha tasnia ya habari iwe bora kwa
mustakabali wa nchi yetu” amesema Gwandu.Amesema APC kupitia mradi wa Alternative Media imefanya utafiti na kupata maoni ya wanahabari na wadau nchini ambao kwa pamoja wanaiomba Serikali ibadilishe sheria  na kanuni mbalimbali  ambazo zimekuwa vikwazo vikubwa katika tasnia ya habari nchini ikiwemo  kanuni namba 4 ya maudhui mtandaoni inayotaka kila anayeanzisha chombo cha habari mtandaoni (online media), kulipa kiasi cha Tsh1100,000 fedha ambazo ni nyingi kulingana na uwezo wa wanahabari nchini.
Aidha, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kazi
kubwa anayofanya kwa kutekeleza miradi mingi kwa manufaa ya Watanzania
na kusisitiza kwa mwenye macho haambiwi tazama.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe akipokea kipeperushi cha majukumu ya uongozi wa Arusha Press
Club mara baada ya kumaliza kikao na uongozi huo kuhusu namna bora ya
kutekeleza majukumu yao ya kihabari leo Jijini Dodoma.awali akiwasilisha maoni ya wanahabari kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria na kanuni mbalimbali Wakili James Marenga alimweleza Waziri kuwa katika utafiti uliofanywa  na Arusha Press Club umeweza kubaini mambo mengi ambayo yamekuwa kikwazo kwa wanahabari lakini kwa kuanzia wamebainisha mambo machache ambayo ni pamoja na kuiomba Serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sheria kama ifuatavyo; 


Sheria
ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970 sura ya 47 inatakaza mwandishi wa habari
kuchapisha taarifa yoyote ambayo ni SIRI lakini haijafafanua taarifa hizo
ni zipi. Serikali  inashauriwa
kubainisha taarifa hizi ili kuondoa mgogoro usiokuwa wa lazima. Lakini pia
kutamka Waziri wa Usalama ni yupi tofauti na sasa
.


 • Sheria
  ya haki na kinga ya Bunge ya mwaka 1988 kifungu cha 27 hakijataja
  waandishi wa habari kama sehemu ya haki yao kikatiba kuhudhuria bunge na
  badala yake wamekuwa wakiingia kwa upendeleo.  Serikali inashauriwa kulishauri bunge kubadilisha kifungu hiki na
  kutaja waandishi wa habari kama ni haki yao kuhudhuria bunge na kuchukua
  habari.

 • Sheria
  ya magereza ya mwaka 1967, kifungu cha 91(20) kimekataza afisa yoyote wa
  magereza kutoa taarifa bila idhini ya Kamishna Mkuu wa Magereza. Serikali
  inashauriwa kuruhusu afisa yoyote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya
  kutoa taarifa kwa waandishi wa habari muda na wakati wowote wanapohitaji taarifa
  .

 • Sheria
  ya huduma za habari ya mwaka 2016 kifungu cha 5(4), haijalazimisha
  kutolewa kwa taarifa zaidi ya kusema ni haki ya kila mtu kutoa au kupokea
  taarifa. Serikali inashauriwa kuweka msisitizo katika kifungu hiki kuwa ni
  haki ya mwandishi kupata taarifa bila kikwazo chochote
  .

 •  Kanuni ya adhabu (Penal code) kifungu cha
  75-76, hakijaweka ulinzi wa waandishi wa habari wawapo katika mikutano
  isiyokuwa halali na badala yake inatoa ruhusa kwa afisa wa Serikali
  kupokonya vifaa vya kazi kwa mwandishi atakayekuwa katika eneo hilo.  Serikali inashauriwa kutunga sheria
  inayompatia ulinzi mwandishi wa habari endapo atakuwa akifanyakazi katika
  mazingira ya namna hiyo na kuondoa adhabu iliyotajwa kwa kuwa yeye yupo
  kazini.