Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Serikali imeazimia kuongeza kiwango cha wastani cha kimataifa cha uboreshaji wa ufanisi wa nishati ifikapo mwaka 2030 ili kuhakikisha inatimiza lengo lililowekwa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa matumizi bora ya nishati nchini, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Dotto Biteko amesema kuwa, mkutano huo uliojumuisha viongozi wa fikra, wataalam na wadau katika nyanja ya ufanisi wa nishati unategemewa kuleta mabadiliko na mafanikio kwa mustakabali wa nchi na bara zima la afrika katika kufikia masuluhisho ya nishati safi.
Aidha ameongeza kwamba, takwimu zawakala wa kimataifa wa nishati (IEA) inaonyesha kuwa maendeleo ya kila mwaka yanahitaji kuongezeka kutoka asilimia 2 ya sasa kwa mwaka hadi asilimia 4 ili kufikia lengo kuu.
“Niikumbushe jamii kuwa ufanisi wa nishati ni kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya yenye tija, kupunguza gharama za uendeshaji na kutoa uokoaji mkubwa wa muda mrefu, hivyo ufanisi wa nishati sio kikwazo bali kichocheo cha ukuaji wa uchumi na utulivu, ameendelea kufafanua
” Suluhu safi na zenye ufanisi zaidi za kupikia hushughulikia afya ya umma kwa kupunguza uzalishaji unaodhuru na kuchangia usawa wa kijinsia hususan wanawake na wasichana ambao ndio hasa huguswa moja kwa moja na matumizi hayo, hivyo Wizara imejipanga kikamilifu kufikia malengo ya mkakati, tushikane mkono kwa pamoja ili kujenga uchumi bora zaidi wa nishati” amesema Dkt Biteko.
Sambamba na hayo amezitaja changamoto zinazokabili juhudi hizo kuwa ni kupata ufadhili wa kutosha, kuratibu juhudi katika sekta zote, kuhakikisha utayari teknolojia na kudumisha kujitolea kwa nguvu ni vikwazo ambavyo lazima vishughulikiwe.
“Kipekee napongeza ushirikiano wa Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland kwa umakini wao, msaada wa taasisi hizi unasisitiza nguvu ya ushirikiano wa kimataifa na kujitolea kwa pamoja kwa ulimwengu wa kijani” ameeleza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eng. Felchesm Mramba ameitaka jamii kutumia nishati safi ili kuokoa gharama zisizo za lazima.
Amesisitiza matumizi ya vifaa vya umeme vyenye ubora uliothibitishwa, hatua itakayounga mkono jitihada za kufanikisha ufanisi wa niahati bora.
“Tumetengeneza mkakati wa masuala ya nishati kwa ubora na uangalifu ili kwenda sambamba na vifaa vinavyoingia nchini kuwa na ubora, katika kutekeleza hili tunafanya kazi kwa karibu na shirika la viwango nchini (TBS), NBS, EWURA na wadau wengine” amesema Mramba.
Vilevile Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa kwa niaba Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, ametaja umuhimu wa nishati safi katika Mkoa wa Arusha kutokana na shughuli za kibiashara na utalii zinazofanyika Mkoani humo.
“Mkoa wetu kama nilivyoanisha shughuli zake tunapitia changamoto za kimazingira na matumizi yasiyofaa, hivyo naona mkakati huu utakuwa jawabu la kukuza uchumi wa mmoja mmoja na taifa kwa ujumla” ameeleza Mtahengerwa.
Mmoja wa wadau wa matumizi ya nishati safi ya umeme jijini arusha Ahadi Fabiano ameipongeza serikali kwa mkakati huo na kubainisha kwamba maisha bila nishati hayawezekani.
“Nafurahi nikiona nishati safi inatiliwa mkazo, unajua kwa maisha ya watu wengi wanategemea nishati kujipatia kipato, hivyo naona kabisa nia njema ya serikali yetu kutaka kuinua uchumi na kuharakisha maendeleo yetu” amepongeza Ahadi.