OFISI YA RC ARUSHA, MATATANI KUVUJISHA SIRI ZA WANANCHI

  • Barua iliyomtuhumu Askofu Issangya kupora ardhi, kufunga na kubomoa kanisa la Pentekoste yakutwa kijiji cha sakila
  • Askofu amshtaki aliyeandika barua akidai alipwe Milioni 500

Na Seif Mangwangi, Arusha

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imelalamikiwa kuvujisha siri za watu wanaofikisha malalamiko yao ndani ya ofisi hiyo baada ya moja ya barua iliyofikishwa katika ofisi hiyo ikimlalamikia Askofu wa Kanisa la International Evangelism Center Sakila, Dkt Eliud Issangya kuonekana katika ofisi za Kijiji cha Sakila.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Augustino Meshack Nnko mmoja wa wazee wa baraza la kanisa la Pentekoste Arumeru tawi la Sakila amesema Oktoba 18, 2024 walimuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Arusha, iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘Kujibu barua ya Baba Askofu Dkt Iliud N. Issangya ya tarehe 7/10/2024 yenye kumbukumbu na.29/07/2030’  ambapo katika aya ya kwanza ya barua  hiyo iliandikwa kwamba ni kumjibu Askofu Eliud Issangya barua yake aliyomuandikia Mkuu wa Mkoa akidai kuwa hatofika kwenye shauri dhidi ya Agustino Nnko na kutoa sababu zake.

Mzee Augustino anasema kabla ya Mkuu wa Mkoa kumpatia majibu ya barua yake, alishangazwa kuitwa na viongozi wa ofisi za kijiji cha Sakila wakiongozwa na Mwenyekit,  Richard Mbise na Mtendaji wa kijiji Jophace S. Lekagi wakimtuhumu kumkashifu Askofu Dkt Eliud Issangya kupitia barua yake aliyomuandikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

“Nilishangazwa sana na tuhuma nilizopewa baada ya kuitwa na uongozi wa kijiji cha Sakila, walinihoji kama ni mimi ndiye niliyeandika barua hiyo nikawaeleza ni kweli, na mimi niliwahoji wameipata wapi barua hiyo wakati nilipeleka ofisini kwa Mkuu wa Mkoa  na sio ofisi ya Kijiji, wakasema wameiokota ofisi ya kijiji baada ya mtu mmoja asiyejulikana kuitupa ndani ya ofisi na kukimbia,”anasema Mzee Augustino Nnko.

Anasema baada ya kikao hicho ambacho pia Diwani wa kata ya Kikatiti, Kisali Nyiti alihudhuria, alipokea wito wa kisheria kutoka kwa wakili wa Askofu Dkt Issangya, Salehe Baraka Salehe wa kampuni ya uwakili ya Fair Fax Attorney ikimtaka kumlipa Askofu Issangya kiasi cha Milioni 500,000 kama fidia ya kumchafua na kumshushia heshima yake na kwamba fedha hizo zilipwe ndani ya siku 7.

Kanisa la Pentecoste Sakila linalodaiwa kuvunjwa na Dkt Eliud Issangya wa kanisa la international Evangelism Center na juu ni Mwanzilishi wa Kanisa hilo Marehemu Mzee Nnko.

Aidha wito huo ulimtaka Mzee Nnko kuandika barua na kuisambaza katika mamlaka mbalimbali za Kiserikali na katika jamii kufuta, kutengea na kubatilisha kashfa zote alizoandika dhidi ya mteja wao, Dkt Eliud Issangya ndani ya siku 7.

“Unatakiwa uape na kutoa ahadi kuwa utaacha kumkashifu au kutoa maneno ya kumkashifu , kero, matusi , uongo na uzushi kwa mteja wetu ndani ya siku 7,” ulisema wito huo wa kisheria.

Mzee Nnko anamtuhumu Askofu Issangya kufunga na kubomoa jengo lote la kanisa la Pentecoste tawi la Sakila ambalo alilijenga yeye pamoja na Baba yake Marehemu na kuweka askari kulinda eneo hilo akizuia mtu yoyote kuingia katika eneo hilo na kulazimika kujenga banda na kuezeka maturubai ili kuendelea na ibada.

“Askofu issangya amekuwa mtu katili sana, amefunga kanisa na kubomoa jengo lote la kanisa ambalo nilijenga mimi na Marehemu Baba yangu na baadae waumini kulimalizia, nimeshalalamika sehemu nyingi na ameshaamriwa arejeshe aneo hilo lakini amekuwa akikaidi,”anasema mzee Nnko.

Hata hivyo Mzee Nnko anasema baada ya siku 7 kupita bila kutekeleza amri aliyopewa na ofisi ya wakili wa Askofu Issangya, ghafla alipokea barua ya wito mahakamani akitakiwa kufika mahakamani kujibu tuhuma za madai ya kashfa alizozitoa dhidi ya askofu Dkt Eliud Issangya.

Askofu Issangya kupitia kwa wakili wake kampuni ya uwakili ya Fair Fax Attorney, amemfungulia Mzee Augustino Meshack Nnko kesi ya madai nambari 2735 ya 2024 katika mahakama kuu Mkoa wa Arusha, ikimtaka mzee Nnko kumlipa Askofu Dkt Issangya fidia ya Milioni 500 kwa kumkashifu pamoja na Milioni 100 kwa kumnyanyapaa, kumsababishia mshtuko wa akili, na kumshushia hadhi yake katika jamii ambapo anatakwia kufika mahakamani hapo Machi 25 mwaka huu 2025 kujibu tuhuma zinazomkabili.   

Marehemu Askofu Nickson aliyekuwa askofu wa kanisa hilo akiwa na waumini wake nje ya kanisa la mabanzi walilojenga baada ya kanisa kuu kubomolewa

Kufuatia kesi hiyo, Mzee Augustino Nnko anamuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kuingilia kati suala hilo kwa kuwa yeye anachokidai ni haki yake pamoja na waumini wake ambacho kinapokonywa kwa nguvu na Askofu Dkt Eliud Issangya.

Aidha anahoji uhalali wa afisa Mtendaji pamoja na Mwenyekiti wa kijiji kuhoji barua ambayo ilipaswa kumfikia Mkuu wa Mkoa na badala yake wao wakaanza kuihoji na kumgeuzia kibao mlalamikaji katika barua hiyo na kumtuhumu kueneza chuki na visasi bado na tuhuma za uongo dhidi ya Askofu jambo ambalo sio kweli.

Akizungumzia malalamiko ya Mzee Nnko dhidi ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuvujisha barua yake, Afisa Tawala Mkoa wa Arusha, Mussa Missaile amesema hawezi kuwa na majibu kuhusiana na madai hayo ya Mzee Nnko kwa kuwa suala hilo ni geni kwake na kumtaka afike ofisini ili aweze kumsikiliza.

Askofu Issangya alipotafutwa ofisini kwake hakuweza kupatikana kwa kuwa yuko  nje ya nchi na hata wakili wake,  Salehe Baraka alipotafutwa kupitia simu yake nambari 0713962812 simu yake iliita bila kupokelewa kwa zaidi ya mara tano.