Picha : abiria wanusurika kifo hiace ikiteketea kwa moto stendi ya mabasi soko kuu mjini shinyanga



Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog



Abiria ambao idadi yao haijajulikana
wamenusurika kuungua baada ya gari aina ya Hiace yenye namba za usajili
T998 AAP inayofanya safari zake Shinyanga kwenda Maswa mkoani Simiyu
kuteketea kwa moto.



Tukio hilo limetokeo leo Ijumaa Novemba 29,2019 majira ya saa nane na
nusu mchana wakati abiria wakiwa wamepanda kwenye Hiace hiyo katika
Stendi ya Mabasi ya Soko Kuu Mjini Shinyanga wakijiandaa kuanza safari
kuelekea Maswa mkoani Simiyu.
Dereva wa Hiace hiyo aliyejulikana kwa jina Basu Gereja amesema chanzo
ni kupasuka kwa Betri na kusababisha gari hilo kuwaka moto.
“Chanzo ni Betri kulipuka,tumefanya utaratibu wa kuwatoa abiria kwenye
gari kisha kupiga simu Zimamoto kwa ajili ya msaada ambao wamefika na
kusaidia kuzima moto huu,gari ilikuwa inatoka Shinyanga kwenda
Maswa”,amesema Basu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na Malunde1 blog
wamesema kuwa dereva alikuwa amewasha gari akijiandaa na safari ndipo
ghafla walipoona gari linawaka moto ndipo utaratibu wa kuwatoa abiria
ukaanza kufanyika huku abiria wengine wakitokea madirishani kwa sababu
mlango uligoma kufunguka.
Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga
Edward Lukuba (Afisa Oparesheni Mkoa wa Shinyanga) amesema wamepata
taarifa za kuteketea gari kwa kuchelewa na kukuta gari hilo linaungua na
kufanikiwa kuzima moto huo huku akiwasisitiza wananchi kujitahidi kuwa
wanatoa taarifa mapema pindi majanga yanapotokea.

Hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa kufuatia ajali hiyo.

Maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiendelea kuzima moto uliokuwa
unateketeza Hiace katika Stendi ya Mabasi Soko Kuu Mjini Shinyanga –
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga
Edward Lukuba (Afisa Oparesheni Mkoa wa Shinyanga) akiwa eneo la tukio