Picha : wadau wa maji mkoa wa tabora watembelea chanzo cha mradi wa maji ya ziwa victoria

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Wadau wa Maji mkoa wa Tabora wamefanya
ziara kwenye chanzo cha mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria cha
Ihelele wilayani Misungwi mkoani Mwanza ili kujionea na kujifunza namna
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira katika mji wa Kahama na Shinyanga(
Kahama Shinyanga Water Supply and Sanitation Authority(KASHWASA)
inavyozalisha na kusambaza maji katika maeneo mbalimbali nchini
Tanzania.

Wadau hao wa maji wakiwemo viongozi wa
serikali ya mkoa na wilaya,madiwani,viongozi wa vyama vya siasa na dini
na wananchi wa Tabora wametembelea chanzo cha mradi wa maji ya ziwa
Victoria Jumanne Januari 14,2020.

Wakiwa Ihelele wadau wa maji
wameshuhudia jinsi maji yanavyotolewa katika Ziwa
Victoria,yanavyotibiwa, yanavyochujwa na kusukumwa kwenda kwenye Tenki
kubwa la maji lenye ujazo wa lita Milioni 35 za maji lililopo kwenye
mlima Mabale wenye urefu wa mita 400 ambapo pia wametembelea tenki hilo.

Akitoa taarifa ya Mradi huo,Mkurugenzi
Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa alisema lengo la
kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2009 ukigharimu shilingi Bilioni 251 za
mapato ya ndani ya nchi ilikuwa ni kutatua changamoto ya maji katika mji
wa Shinyanga na Kahama na sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo
mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Tabora.

Alisema hivi sasa wanahudumia wateja
saba ambao ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga Mjini
(SHUWASA), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga Mjini
(KUWASA),Ngudu,Kishapu,Maganzo,Mgodi wa Mwadui na kusambaza maji katika
kamati 64 maji Misungwi na Kwimba na kamati za wateja wadogo katika
halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kahama Mji na Msalala.

Mhandisi Mgeyekwa alisema hivi sasa
wanaendelea na ujenzi wa mradi wa Maji katika Mkoa wa Tabora ambao hadi
kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Bilioni 600 na tayari maji yamefika
katika tenki la maji Ushirika Nzega lenye ujazo wa lita  milioni 2.5,
Kilichobaki ni kuyaweka katika mfumo wa usambazaji.

Alisema miradi inayoendelea kujengwa itafikisha uzalishaji maji hadi lita milioni 64 ifikapo Juni,2025.
“KASHWASA haipati ruzuku kutoka serikalini lakini serikali inawekeza kwenye miradi mikubwa ya maji”,alisema.

“Mapato yetu kwa mwezi ni shilingi
Bilioni 1.1 ambapo asilimia 60 inakwenda kwenye gharama za umeme na
dawa,asilimia 40 inayobaki inakwenda kwenye mishahara ya watumishi wetu
na mambo mengine”
,alisema Mhandisi Mgeyekwa.

Alisema kutokana na hali hiyo sasa
KASHWASA inajitegemea kwa asilimia 100 kwa upande wa gharama za umeme na
madawa ya kutibu maji na mishahara ya watumishi hivyo inapata ruzuku
kutoka serikalini asilimia 20 tu.

“Changamoto iliyopo ni wateja
kutotumia maji. Uwezo wa mtambo wetu ni kuzalisha lita milioni 80 kwa
siku lakini kwa mahitahi ya sasa tunazalisha lita milioni 43 tu kwa
siku.Tunahitaji wateja wengi zaidi ili watumie maji tunayozalisha”,
aliongeza Mhandisi Mgeyekwa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu
Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora , Rukia Manduta alisema wamepokea kwa
furaha mradi wa maji ya Ziwa Victoria akibainisha kuwa watakuwa wateja
wazuri wa KASHWASA.

Manduta alitumia fursa hiyo kuwaomba
wananchi wa Tabora kuwa walipaji wazuri wa Ankara za maji,kuwa walinzi
wa miundo mbinu ya maji ili kuepuka upotevu wa maji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya
Igunga,John Mwaipopo aliipongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa maji
ya Ziwa Victoria na kuwataka wananchi kuyalinda na kuyatunza maji hayo
pindi yatakapofika mkoani Tabora ili kuondokana na changamoto ya maji
ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji
na Usafi wa Mazingira katika mji wa Kahama na Shinyanga (Kahama
Shinyanga Water Supply and Sanitation Authority( KASHWASA) Mhandisi
Joshua Mgeyekwa akiwakaribisha wadau wa maji kutoka mkoa wa Tabora
walipotembelea chanzo cha mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria cha
Ihelele wilayani Misungwi mkoani Mwanza Januari 14,2020. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi
Joshua Mgeyekwa akiwaelezea wadau wa maji kutoka Tabora kuhusu Mradi wa
Maji ya Ziwa Victoria unaosimamiwa na KASHWASA.
Wadau wa maji kutoka mkoa wa Tabora
wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Joshua Mgeyekwa
wakati akitoa taarifa ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *