Prof. kabudi akutana na kufanya mazungumzo na mwakilishi wa unicef

Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini
Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar
es Salaam.

Waziri Kabudi amemweleza Bi. Shalini Bahuguna kuwa UNICEF imekuwa na
mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.

“Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za
maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na
tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho”. Amesema Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi amemueleza Bi. Bahuguna kuwa tangu mwaka 2016 Serikali ya
Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa kuboresha sekta za
elimu na afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa
huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na
kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam,
Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia watoto (UNICEF) nchini, Bi. Bahuguna amesema kuwa UNICEF
itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania
inaendelea
kulinda haki za watoto.

“Haki za watoto katika taifa ni jambo muhimu sana, hivyo UNICEF
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki za
watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu”. Amesema Bi.
Bahuguna.