Prof. msoffe aelezea mikakati yake mipya ya uendeshaji narco

 

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za
Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe akisaini kitabu cha wageni mara baada
ya kuingia kwenye ofisi za NARCO jijini Dodoma kwa ajili ya kukabidhiwa
ofisi leo July 1,2021.

Aliyekuwa Meneje Mkuu wa Kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO), Bw. Masele Shilagi (kulia) akimkabidhi gari
Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Prof. Peter Msoffe (katikati) wakati wa
makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Stephen Michael.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za
Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe (kulia) akipokea taarifa ya
makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw.
Masele Shilagi (kushoto). Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Stephen Michael akishuhudia
makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye Ofisi za NARCO jijini Dodoma.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za
Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe (kulia) akipeana mkono na aliyekuwa
Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Masele Shilagi baada ya
kukabidhiana ofisi jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Stephen Michael akizungumza na viongozi
na watumishi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa mara baada ya kumalizika kwa
makabidhiano ya ofisi jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Stephen Michael (wa tatu kutoka
kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) mara baada ya kukamilika kwa
makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika jijini Dodoma.

Meneja Mkuu wa Kampuni za Ranchi za
Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe ametaja mikakati itakayosaidia kampuni
hiyo kuweza kujiendesha kibiashara Zaidi.

Prof. Msoffe ameibainisha mikakati
hiyo baada ya kumalizika kwa kikao cha makabidhiano ya ofisi na
aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO, Masele Shilagi kilichofanyika leo
July 1,2021 jijini Dodoma.

Akizungumzia mikakati hiyo, Prof.
Msoffe amesema kuwa serikali inataka kampuni hiyo iwe kitovu cha umahiri
wa masuala yote yanayohusu ranchi. Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa
ni lazima kampuni ijipange katika uzalishaji wa nyama ya kutosha iliyo
bora, uzalishaji wa mifugo iliyo bora, kutoa mafunzo kwa wataalam na
wafugaji, kujiendesha kibiashara na kuweza kupeleka gawio serikalini.

Aidha, amesema ana matarajio makubwa
kuwa hayo yataweza kutekelezeka kwa kuwa yeye ameikuta kampuni ikiwa
inaendelea kuimarika hivyo kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wa
kampuni wataweza kutekeleza mikakati hiyo ambayo itawasaidia kuweza
kutimiza azma ya serikali kwa kampuni hiyo.

Naye Masele Shilagi ambaye alikuwa ni
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa amesema kuwa kampuni
imekuwa ikiendelea kuimarika kimapato ambapo iliweza kujiendesha bila
kutumia ruzuku kutoka serikalini. Pia wameweza kusimamia mapato na
matumizi ambapo kampuni imekuwa ikipata hati safi.

Lakini pia amesema kampuni imeweza
kupima baadhi ya ranchi zake na kushughulikia migogoro iliyokuwepo
ikiwemo ya uvamizi wa wananchi kwenye maeneo ya ranchi. Aidha, Masele
amewashukuru viongozi na watumishi wa NARCO kwa ushirikiano waliompatia
kipindi cha uongozi wake na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa
Meneja Mkuu mpya.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya
Uzalishaji na Masoko, Stephen Michael amesema kuwa viongozi na
watendaji wanao wajibu wa kujipanga vizuri ili kuhakikisha malengo na
matarajio ya serikali yanatimizwa. NARCO inazo fursa nyingi kwenye
uzalishaji wa nyama bora, mifugo bora, malisho na utoaji wa elimu kwa
wafugaji.

Michael amesema katika kuhakikisha
fursa zinatumika na mapato yanaongezeka kama serikali ilivyopanga, ni
lazima uongozi uone namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi lengo
likiwa ni kuongeza uzalishaji na kuongeza mapato.