Profesa mbarawa azipa miezi mitatu mamlaka za maji nchini kufungia wateja wao mita za maji

Na Mwandishi Wetu 

Mamlaka za maji zinazotumia bei za
kukadiria (flat rates) kote nchini zimepewa miezi mitatu kuhakikisha
zinawafungia dira za maji wateja wao wote ili kila mteja alipe gharama ya maji
kwa kiasi alichotumia.
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb)
akikata utepe kuzindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya
Kikubiji, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.

Waziri wa
Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akifungua bomba la maji la mradi wa
Shilima wakati wa uzinduzi wa mradi huo Septemba 14, 2019
Waziri wa
Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) (mbele katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya viongozi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa maji Shilima.
Baadhi ya
wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa mradi
wa maji wa Shilima

Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa (Mb) alitoa agizo hilo  alipokuwa akizindua mradi wa
maji wa Kijiji cha Shilima Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba Mkoani
Mwanza. 

Waziri Mbarawa alisema Serikali
imetenga Bilioni moja kusaidia mamlaka za maji ambazo hukadiria matumizi ya maji wateja
wake badala ya kutumia dira ya maji ili kuepuka kumbebesha mteja mzigo usiyo
kuwa wake. 
Waziri
Mbarawa vilevile ameziagiza
mamlaka za maji za mikoa kuhakikisha zinadhibiti upotevu wa maji kwani
maji mengi yanapotea kabla ya kufika kwa wananchi sambamba na
kuongeza mtandao wa maji ili kuwaunganisha wananchi wengi zaidi.
Akizungumzia mradi wa maji wa
Shilima, Profesa Mbarawa alisema u
jenzi wake ni utekelezaji wa Sera ya
Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwapatia  huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85
wakazi wote waishio vijijini ifikapo mwaka 2020.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni
awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Vijiji vya Shilima,
Mhande na Izizimba.
Alibainisha kwamba mradi wa maji wa
Shilima ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika katika kipindi
cha miezi sita. Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa Mkandarasi aliyekuwa anautekeleza pamoja na
usimamizi mbovu haukuweza kukamilika kwa wakati. 
Waziri Mbarawa aliwapongeza wote
walioshiriki kwenye ujenzi wa mradi kwa namna mbalimbali na kwa ushirikiano
waliotoa kwa kipindi chote cha ujenzi wake hadi unakamilika kwa
wakati kama alivyokuwa ameelekeza.
Akizungumzia
ujenzi wa mradi huo,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini
Mwanza (MWAUWASA) ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi,
Mhandisi Anthony Sanga alisema walizingatia agizo la Waziri Mbarawa na
kwamba
mradi huo ulikamilka tarehe 25 Agosti, 2019 kabla ya muda uliyokuwa
umeelekezwa.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA
Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Matundalo alisema kuwa Kijiji cha Shilima kina
wakazi wapatao 7,526 ambapo mradi huu wenye magati 35 una uwezo wa kuhudumia
wakazi 8.750 ikiwa ni wastani wa watu 250 kwa kila gati.

Waziri Mbarawa tarehe 3 Julai, 2019
akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kwimba alitoa ahadi ya kukamilisha mradi
huo kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha
Shilima wanapata maji katika kipindi cha miezi miwili, yaani hadi kufikia
tarehe 3 Septemba, 2019, ahadi ambayo hata hivyo ilikamilika tarehe 25 Agosti,
2019 siku tisa kabla ya tarehe ya makubaliano.