Rais magufuli abatilisha ufutaji wa shamba la ekari 1000 mvomero

Na Munir Shemweta, WANMM MVOMERO

Raisi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amebatilisha
pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa ekari 1000 lililopo Kidunda
wilayani Mvomero mkoani Morogoro linalomilikiwa na Cecilia George
Rusimbi.

Uamuzi
wa Dkt Mafuli kubatilisha ufutaji shamba hilo unatokana na kubainika
kuwa pendekezo lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo kwa madai ya
kutoendelezwa kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki wake.

Akitangaza
uamuzi huo wa Raisi jana wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, baada ya kufuatilia mashamba
yaliyopendekezwa kufutwa Dkt Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa za
kufuta shamba Cecilia hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha
pendekezo lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.

Kufuatia
hali hiyo Waziri Lukuvi aliwaonya Maafisa ardhi nchini kuhakikisha
wakati wa kufanya zoezi la ukaguzi/Upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa
wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo
kwa upendeleo au kumuonea mtu.

Hata
hivyo, Waziri wa Ardhi alisema, utendaji kazi katika wilaya ya Mvomero
umekuwa wa hovyo na usiozingatia maadili jambo linalopelekea wilaya hiyo
kuongoza katika mkoa wa Morogoro kuwa na migogoro mingi ya ardhi
sambamba na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya ofisi ya ardhi.

‘’Baadhi
ya watumishi katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero
mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapima wakati hamkuajiriwa kwa nafasi
hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na kuwaumiza wananchi’’ alisema Lukuvi

Kwa
upande wake Cecilia George Rusimbi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa
kubatilisha ufutaji shamba lake na kuuelezea uamuzi huo kuwa 
umezingatia haki na kusikia kilio chake ambapo alisema umempa faraja
baada ya kuhangaika sana kuhusiana na shamba hilo.

‘’
Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa muda mrefu
na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa
kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi’’
alisema Cecilia.

Waziri
Lukuvi ameagiza shamba hilo la kilimo cha Michikichi, Mitiki na Bamboo 
kupangwa upya na mmiliki wake kupatiwa hati kulingana na upimaji
utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza kwa mujibu wa sheria.

Sambamba
na sakata la shamba la Cecilia, Lukuvi aliagiza kupunguzwa ukubwa wa
Shamba Sangasanga na Lubango lililodaiwa kuwa na ukubwa wa ekari 1,103
wakati uhalisia wa shamba hilo ni ekari 500 na kuagiza mmiliki wake
kurudisha hati ili apatiwe hati ilinayolingana na uhalisia wake na ekari
603.5 zilizoongezwa zitabaki kuwa ardhi ya akiba.

Naye
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl Mohamed Utaly alieleza kuwa wilaya yake
ina tatizo kubwa la migogoro ya ardhi pamoja na jitihada kubwa
inayofanywa na ofisi yake kukabiliana na tatizo hilo na kuongeza kuwa
mingine inachochewa na uhamasishaji unaowafanya wananchi kukata tamaa.

Katika
hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi alitembelea ofisi ya Ardhi katika halmashauri ya Mvomero na
kubaini ‘madudu’ katika ofisi hiyo ambapo alibaini baadhi ya majalada ya
wananchi waliomba kumilikishwa ardhi tangu mwaka 2012 katika
halmashauri hiyo kushindwa kupatiwa hati huku.

Hali
hiyo ilimfanya Waziri Lukuvi kumuagiza Kaimu Kamishana Msaidizi wa
Ardhi Kanda Maalum ya Morogoro Erick Makundi kuhakikisha wale wote
walioomba hati na kutumiza vigezo vya kupatiwa hati wanapatiwa kufikia
mwezi ujao Desemba 2019. Pia ameagiza kufuatiliwa majalada 300 ambayo
wamiliki wake wamekamilisha taratibu za kupatiwa hati lakini
hawajapatiwa.

Sambamba
na hilo Lukuvi aliagiza wafanyakazi wa ofisi ya ardhi katika
halmashauri hiyo wanaojitolea kutosaini nyaraka zozote za ardhi kwa kuwa
baadhi yao wamekuwa wakishiriki kutoza tozo kwa gharama za juu za
shilingi 50,000 wakati gharama halisi ni 20,000.