Rais magufuli afanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri… simbachawene achukua nafasi ya kangi lugola

Rais John Magufuli amemteua mbunge wa
Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo,
George Simbachawene akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Simbachawene anachukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa. 
Hayo yameelezwa leo jioni Alhamisi Januari 23, 2020 na katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi. 

Mabadiliko hayo madogo ya baraza la
mawaziri yamefanyika baada ya leo asubuhi katika hafla ya uzinduzi wa
nyumba za askari wa Jeshi la Magereza zilizopo Ukonga, Dar es Salaam,
Rais Magufuli kueleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Lugola na
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye
ambaye naye uteuzi wake umetenguliwa, huku ikielezwa nafasi yake
itajazwa baadaye. 
Katika uteuzi huo, Rais Magufuli
amemteua aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja
Jenerali Jacob Kingu kuwa balozi. 
Katika hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo,
Magufuli alisema Meja Jenerali Kingu aliandika barua ya kujiuzulu na
alimkubalia, kueleza kuwa amemheshimu kwa uamuzi wake huo. 
“Leo Rais Magufuli amemteua Zungu kuwa
Waziri anayeshughulikia muungano na mazingira na kumhamisha Simbachawene
kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua nafasi ya Lugola ambaye uteuzi
wake umetenguliwa,” amesema Balozi Kijazi. 
Amesema Rais Magufuli pia amefanya
uteuzi wa mabalozi watatu watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi
mbalimbali baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao, kufikisha umri wa
kustaafu. 
“Amemteua Meja Jenerali Kingu ambaye alikuwa katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu jana Januari 22, 2020.” 
“Amemteua Dk Steven Simbachawene kutoka
ofisi ya rais Ikulu na kamishna Jenerali Faustine Kasike ambaye kabla ya
uteuzi huu alikuwa kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, nafasi ya
Kasike itajazwa baadaye. Vituo vya kazi vya mabalozi hawa watatu
vitatangazwa baadaye,” amesema balozi Kijazi. 
Balozi Kijazi amesema Rais Magufuli
amewaongezea muda mabalozi saba wa Tanzania, akiwemo Asha Rose Migiro
ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Uingereza.