Rais magufuli akutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa aalco na naibu waziri wa mambo ya nje wa china – ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na viongozi wa Taasisi ya Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO) ambao wanahudhuria mkutano wa 58 unaofanyika hapa nchini kwa siku 5 ukiwakutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama 49 na mashirika mbalimbali.Viongozi
wa AALCO waliokutana na Rais Magufuli ni Rais wa AALCO, Balozi Dkt.
Augustine Mahiga (Waziri wa Sheria na Katiba, Tanzania), Makamu wa Rais
wa AALCO Prof. Mohamad Shalaldeh (Waziri wa Sheria wa Palestina), Katibu
Mkuu wa AALCO Prof. Kennedy Gastorn (Tanzania) na Naibu Makatibu Wakuu
wa AALCO watatu ambao ni Yukihiro Takeya (Japan), Wang Liyu (China) na
Dr. Ali Garshasbi (Iran).

Rais
Magufuli amewashukuru na kuwakaribisha wajumbe wa AALCO nchini Tanzania
na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua kazi inayofanywa na taasisi
hiyo tangu ijiunge nayo mwaka 1965 na kuwa mwanachama kamili kuanzia
mwaka 1973.

Rais
Magufuli amesisitiza umuhimu wa AALCO kutekeleza malengo ya taasisi
hiyo kama alivyoelezwa na viongozi hao, na ametoa wito wa kuendelea
kuzitetea nchi wanachama hasa zinazowekewa vikwazo mbalimbali.

Ametolea mfano wa Zimbabwe ambayo imewekewa vikwazo kwa miaka mingi hali inayosababisha wananchi wa Zimbabwe kuteseka.

Rais
wa AALCO Balozi Mahiga na Katibu Mkuu Prof. Kennedy Gastorn
wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupata fursa ya kukutana nae na
wameahidi kuwa AALCO itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya
Asia na Afrika.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Mhe. Amon Mpanju.

Wakati huo huo,
Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC)
Ndg. Guo Yezhou, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais
Magufuli amemuomba Yezhou kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China na
Mwenyekiti wa CPC Mhe. Xi Jinping kwa kutoa tuzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu
wa Tanzania Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim ikiwa ni kutambua mchango wake
katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Rais
Magufuli amemhakikishia kuwa Sera za Tanzania kuhusu China
hazijabadilika na amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China
katika jitihada mbalimbali za maendeleo.

Mazungumzo
hayo yamehudhriwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bashiru
Ally Kakurwa na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke.