Rais magufuli aruhusu makontena yenye mchanga wa madini yarudi katika kampuni ya twiga ili yauzwe

Rais
Magufuli ameruhusu makontena yenye mchanga wa madini ya dhahabu kuuzwa,
akibainisha kuwa tayari mteja amepatikana na ameshatoa kiasi kidogo cha
fedha.


Mwaka
2017 Serikali ya Tanzania iliyashikilia na kuzuia makontena hayo ya
mchanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya
madini yaliyoshindikana baada ya hatua ya kwanza ya uchenjuaji kufanyika
mgodini.


Akizungumza leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika hafla ya utiaji saini
makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick
yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam Rais Magufuli amesema uuzwaji huo
utakuwa na faida kwa sababu ya makubaliano hayo.


“Hata
yale makontena tuliyoyashika sasa fanyeni utaratibu mzuri yarudi katika
Kampuni ya Twiga mtafute wateja. Najua yameshauzwa na mteja yupo na
ameshalipa kiasi fulani. Pamoja na stori kuwa zilikuwa zinapelekwa
kuyeyushwa. Si kweli, yalikuwa yanauzwa.”


Huku akiihakikishia ulinzi kampuni ya Barrick Gold, Rais Magufuli
amesema hakuweza kuvumilia kuwa rais huku rasilimali za Watanzania
zikisombwa.
“Dhahabu iliwekwa Tanzania na siyo sehemu nyingine, aliyeiweka ana
makusudi yake. Kwa hiyo ikisombwa bila Watanzania kupata faida ya hicho
kinachosombwa, hicho ndio kinaumiza .


“Siwezi
kuwa rais na mali inasombwa mnaambiwa ni mchanga, mnakubali na polisi
wanasindikiza. Sasa kama ni mchanga kwanini unalindwa? Na kuzunguka eneo
la mgodi watu wana njaa, hawana elimu, madawa wala maji. Haikuwa sawa,”
alisema na kuongeza;


“Sisi hatupo hapa kugombana na mwekezaji
yeyote, tupo hapa kushirikiana nao katika hali ya kila upande kushinda.
Barrick muwe na uhakika hapa ni mahali pa kukaa, mtakaa hapa leo, kesho
na daima kwa sababu tunaona nyie ni wadau wazuri.


“Nawashukuru Barrick kwa busara, mngeweza kusema tunatumia ‘force’ ila
sina hakika kama mngeichimba hiyo dhahabu. Sina hakika, lakini mmetumia
busara, hiyo ni nzuri sana na serikali yangu itoa ushirikiano mzuri sana
ili mchimbe mpate faida na sisi tufaidike.  Fikiria kutoka ‘share’ ya
sifuri hadi ya 16%, lakini pia faida itakayopatikana ni 50 kwa 50 ni
ushindi mkubwa kwa pande zote mbili.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *