Rais magufuli: sababu ya ndege ya tanzania kukamatwa afrika kusini ni wivu






Rais
Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa sababu ya ndege ya Shirika la
Ndege la Tanzania (ATCL) kukamatwa nchini Afrika Kusini ni wivu,
kutokana na shirika hilo kuanza kuimarika na kuteka masoko mbalimbli
ndani na nje ya Afrika.


Rais
ameyasema hayo leo asubuhi alipokuwa akizindua kituo cha mfumo wa rada
ya kuongozea ndege katika kituo cha Dar es Salaam, ambayo ni moja ya
rada mpya nne zitakazofungwa nchini na kuwezesha kuona na kuongoza ndege
katika anga lote la Tanzania.

“Ukiona hadi watu wanakamata ndege zetu basi ujue shirika letu linafanya kazi vizuri,” alisema Rais Magufuli

Amesema
kuwa licha ya kukamatwa kwa ndege hiyo (ambayo tayari imeshaachiliwa)
ataendelea kuchapaka kazi, huku akitolea mfano kutoka kwenye mashairi ya
wimbo wa kundi la Sauti Sol la Kenya, wimbo unaoitwa Extravaganza ambao
mashairi hayo yanasema, wakifunika, tunafua, wakianika, tunaanua,
wakitufungia milango, wanatukuta ndani.

Rais
ametoa pongezi kwa ATCL kwa namna ambavyo limekuwa likikua huku
akieleza kwamba wakati lilipoanza safari zake lilikuwa likimiliki
asilimia tatu pekee ya soko la ndani, lakini sasa linamiliki asilimia
75. Ameongeza kuwa, tayari shirika hilo limeanza safari za kimataifa, na
karibuni litaanza kwenda China, hivyo ni lazima washindani wake waone
wivu.

Akizungumzia
rada iliyopaswa kununua kipindi cha nyuma, Rais ameonesha kukerwa
kwamba fedha za Watanzania zilitafunwa na watu wachache na rada hiyo
iliyokuwa inunuliwe nchini Uingereza haikusimikwa tena, hivyo mabilioni
ya fedha yakawa yamepotea. Amesema aliwashangaa waliohusika kwenye
sakata hilo kutokujiuzulu, angali wale wa upande wa Uingereza
walijiuzulu.

Baada
ya mifumo mipya ya rada za kuongozea ndege kukamilika kusimikwa,
Tanzania itaweza kuona na kuongoza angala lote la nchi, tofauti na awali
ambapo ilikuwa inaweza kuongoza asilimia 25 pekee ya anga lote.

Kuwa
na uwezo wa kuongoza anga lote kutaongeza mapato ya serikali,
kutaongeza kasi ya ndege kuweza kuruka na kutua katika viwanja vya
Tanzania, hatua itakayoongeza abiria, lakini pia hatua hiyo ni kukidhi
vigezo vya kimataifa.