Rais magufuli: watu wanataka kusajili laini zao lakini zoezi la vitambulisho linacheleweshwa

Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu
wa NIDA kufika Mkoani Morogoro leo na ikiwezekana akae Mkoani humo hata
siku tatu ili kushughulikia tatizo la Watu wengi kukosa vitambulisho
vya Taifa huku Mkoa mzima ukiwa na Ofisi moja pekee ya NIDA.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo akiongea na wananchi wa Msamvu, Morogoro akiwa njiani akielekea mkoani Dodoma.
“Nimemtaka Mkurugenzi Mkuu NIDA afike
hapa Morogoro ashughulikie hii changamoto ya vitambulisho na nataka
huduma hii iende kila Wilaya, haiwezekani Watu wasafiri kutoka Wilayani
kuja Mjini au muwape nauli na hela ya Gesti,na hili litazamwe Nchi nzima
Watu wapewe vitambulisho” amesema.
“Watu wanataka kusajili laini zao za
simu na mambo mengine lakini zoezi la vitambulisho linacheleweshwa na
Watu wachache, suala la NIDA linaenda polepole sana, Mkurugenzi Mkuu wa
NIDA nitahitaji unipe na tathmini ya zoezi lote Nchi nzima”.
Aidha, Rais Magufuli amesisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi hatopanga bei ya mkulima kuuza mazao yake.

“Wengine wanalalamikia bei ya mahindi
kupanda, nataka wakulima washangilie kama bei ya mahindi imepanda,
biashara hii lazima iwe huru, bei ya mahindi itajipanga yenyewe, wakati
wa kuwapangia bei wakulima kwenye mazao yao umekwisha,” amesema Rais
Magufuli.