Sadc: tuko tayari kukabiliana na homa ya virusi vya corona (covid-19)

Waziri
wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari(Hawapo pichani), kuhusu mlipuko wa
ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19) kwa Nchi za SADC katika Mkutano wa
Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam Tanzania.
Katibu Mtendaji 
wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),
Dkt.Stergomena Tax akisoma Taarifa ya Mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Afya wa
SADC  kuhusu kukabiliana na ugonjwa wa
homa ya Virusi vya Corona ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Tanzania.

Waziri wa Afya kutoka Zimbabwe, Dkt. Obadiah Moyo
akifafanua jambo kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19) kwa
Nchi za SADC katika Mkutano wa Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Tanzania.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kutoka Tanzania, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza katika Mkutano wa
dharura kuhusu kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Virusi vya Corona ulifanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam
Tanzania.

Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), imesema imejiandaa kikamilifu kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Virusi vya Corona (Covid-19) ambao umezidi kusambaa duniani na kwamba mikakati madhubuti imeweka tayari kwa kutoa elimu ya kutosha jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo kwa wananchi wa ukanda huo wa Afrika.

 Akizungumza katika Mkutano wa dharura uliofanyika Jijini Dar es Salaam, ambao uliitishwa kujadili hali ya mlipuko wa ugonjwa huo uliohudhuriwa na nchi 10 kati ya 16 za ukanda wa Kusini mwa Afrika, zikiwemo Angola, Congo DRC, Lethoto, Mauritius, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia Namibia na Tanzania, Waziri mwenye dhamana ya Afya kutoka Tanzania, Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa tayari nchi hizo zimefanya maandalizi na sasa zimeingia kwenye hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Tupo hapa leo kujadili hali ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Covid -19), ambao sisi kama nchi wanachama tumekuja kubadilishana taarifa kuhusiana na ugonjwa huu na kuona kama nchi za SADC tumejipanga kukabiliana nao na sasa imeonesha kuwepo na hali ya utayari kwa kila nchi mwanachama”, Alisema Ummy Mwalimu.

 Alibainisha kuwa kati ya Nchi 16 za SADC ni nchi moja tu ambayo mpaka sasa imebainika kuwa na washukiwa wa ugonjwa huo ambayo ni Afrika ya Kusini na nchi zingine ziko salama, lakini walikubaliana kuwa nchi hizo zianzisha utaratibu wa kujipima na kujitathmini badala ya kusubiri tathmini za wadau wa afya.

Katika Mkutano huo, Waziri Ummy alisema nchi hizo zilifikia makubaliano mbalimbali katika kukabili ugonjwa huo ikiwemo hilo la kujitathmini wenyewe, kushirikisha sekta nyingine kama Utalii, Uchumi, fedha pamoja na Uhamiaji, kutoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri wa SADC kutofanya mikutano ya ana kwa ana badala yake njia nyingine zitumike kama vile video conference.

 Aidha aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuweza kupambana na ugonjwa huo kwani mpaka Machi 9, 2020 kumekuwepo na mabadiliko makubwa ambapo maambukiza mapya yamepungua na kufikia watu 28 tu.
 “Ninawashukuru Serikali ya China kwa kudhibiti ugonjwa huu kwani mpaka leo China ina wagonjwa wapya 28 hali hii inaonesha jinsi gani wenzetu wameweza kupambana kwa kiasi kikubwa kwa hiyo sisi kama nchi za SADC tumejipanga kukabiliana na Corona (Covid -19)”, Alisema Waziri Ummy.

 Kwa upande wa Tanzania mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote wa Corona (Covid 19), lakini Serikali imejiandaa kwa kiasi kikubwa kwa kutenga maeneo iwapo ya kuwatibu iwapo wagonjwa hao watapatikana na kwa sasa inajenga eneo la kudumu katika Hospitali ya Mloganzila Jijini Dar es Salaam.

Katika sehemu za kusafiria na kupokea wageni na mizigo ikiwemo Viwanja vya ndege, bandari na maeneo ya mipakani Serikali imeweka vipima joto vya kutambua ugonjwa huo.

Naye Waziri wa Afya kutoka Zimbabwe, Mhe.Dkt. Obadiah Moyo, alisema kuwa Nchi za SADC hususani nchini kwake zimejiandaa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wake jinsi ya kujikinga na kuepukana nao.
 “Tutatoa elimu ya uelewa kwa wananchi wetu kwani elimu hiyo ni muhimu sana kujikinga na ugonjwa huu na tutahakikisha kwamba tunashirikiana na kushirikishana kama nchi za ukanda huu ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu katika nchi nyingine za ukanda huu”, Alisema Waziri Moyo.

 Aidha katika kuwatambua wanafunzi wa Nchi za Kusini Mwa Afrika walioko China, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro alisema kuwa mpaka sasa wanafunzi hao kutoka nchi za SADC wako salama na hakuna aliyeambikizwa.

 “Wanafunzi wa SADC walioko China wako salama kabisa hakuna mwanafunzi yeyote aliyeambukizwa ugonjwa huo, lakini tunataka nchi zetu za SADC zibaki salama tunatakiwa kupata elimu na kuelewa tunachofundishwa kuhusiana na ugonjwa huu”, Alibainisha Dkt.Ndumbaro.
Aliendelea kusema kuwa Dkt.Ndumbaro kuwa Vyombo vya habari ni wadau wakubwa katika kutoa taarifa sahihi kuhusiana na ugonjwa huo, hivyo vinatakiwa kushirikiana na mamlaka husika za afya ili kupata taarifa sahihi ambazo zitawatoa hofu wananchi katika ukanda huo wa Afrika.