Serikali kuvipatia umeme vijiji vyote 56 vya wilaya ya simanjiroNa Beatrice Mosses – Manyara
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medadi Kalemani
amesema serikali itavipatia Umeme vijiji vyote 56 vya Wilaya ya
Simanjiro mkoani Manyara ifikapo mwezi Juni mwaka 2020.

Waziri Kalemani 
aliyasema hayo juzi  katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro
wakati wa ziara yake ya kukagua na kufuatilia utekelezwaji wa upelekaji
umeme vijijini ambapo alisema mkoa wa Manyara  pekee hadi sasa
umeshapokea zaidi ya shilingi Bilioni 31 kwa ajili ya upelekwaji umeme
vijijini.


Waziri wa Nishati Dkt  Medadi Kalemani 
alifika katika Kijiji cha Naepo na Olibili Wilayani Simanjiro  mkoani
Manyara kubwa ni kukagua kazi ya upelekaji umeme kwa wananchi pamoja na
kuwasha umeme shule ya msingi Naepo na shule ya sekondari Shambarai.

“Ndugu zangu wana Simanjiro mna vijiji
56 na vitongoji 275 vyote vinakwenda kupata umeme ifikapo mwishoni mwaka
mwaka ujao Mh. Rais katupatia fedha kwenye mkoa mzima wa Manyara na
Simanjiro ikiwemo  jumla ya sh. Bil. 31.12.

“Rais anawakumbuka kwenye mabarabara,
anawakumbuka kwenye shule lakini pia anawakumbuka kwenye masuala ya
umeme, leo ninyi ni mashahidi shule hii ina zaidi ya miaka 18 ilikuwa
haina umeme”, Alisema Kalemani.

Aidha Dkt Kalemani aliwataka wananchi wa
kijiji cha Naepo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze
kupelekewa umeme kwenye nyumba zao kwa bei ya sh. 27,000 kwani gharama
zingine serikali ilishagharamikia.

“Niwaombe wananchi kama una nyumba yako
wewe na inawezekana ni ya makuti au ni ya majani zote zinastahili
kuwekewa umeme hakuna nyumba isiyofaa kuwekewa umeme na ole wake
Mkandarasi  au  Meneja atakaye ruka nyumba ati kwa sababu ni mbaya
utakuwa wewe mbaya lakini nyumba itabaki salama”, Alisema.

Dkt Kalemani alitoa maelekezo ya kwa
ofisi ya Tanesco mkoani Manyara kufungua dawati la kuwahudumia wananchi
kwani kutoka wilayani hadi kijiji cha Naepo ni zaidi ya km 20.

“Kwa hiyo kituo cha kuandikisha
wanaohitaji kupatiwa umeme kibaki hapahapa msiende wilayani wao
watawafuata hapa hata ukiwa  na pesa kidogo unaiweka hapa ukikamilisha
sh. 27,000 unaunganishiwa umeme”, Alieleza Dkt Kalemani.

Wananchi kwa upande wao wakaishukuru
serikali lakini wakawa na ombi kwa Waziri wa Nishati ili aweze
kuwafikishia umeme kambi ya Chokaa kwa kuwa eneo hilo lipo katikati ya
vijiji ambavyo vina umeme.

Waziri Kalemani akawahakikishia wananchi wa Simanjiro  kuwa kila nyumba na Kitongoji kitapata umeme

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *