Serikali kuwasilisha muswada bungeni wa kuwa na mamlaka ya serikali mtandao

Sehemu ya muonekano wa Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) uliotengenezwa na Wataalam wa ndani wa TEHAMA ambao unatarajiwa unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst.) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na Wataalam wa ndani wa TEHAMA (hawapo pichani) waliotengeneza Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Kieletroniki (eOPRAS) ambayo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst.) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiwahimiza Wataalam wa ndani wa TEHAMA (hawapo pichani) waliotengeneza Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Kieletroniki (eOPRAS) kuhakikisha wanakamilisha utengenezaji wa mifumo hiyo kwa ufanisi ili iwe na manufaa ya kiutendaji Serikalini
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Dkt. Jabir K. Bakari akimuonesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst.) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) namna Serikali Mtandao inavyofanya kazi, wakati waziri huyo alipoitembelea wakala hiyo kuhimiza uwajibikaji.
Na Mwandishi Wetu
Serikali inajiandaa kuwasilisha Muswada Bungeni wa kutungwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 (e-Government Act, 2019) ambayo itawezesha kuundwa kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kusimamia na kuendeleza Serikali Mtandao kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya TEHAMA iliyopo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst.) Mhe. George
Mkuchika (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Wakala ya Serikali Mtandao ili kukagua utendaji kazi wa wakala hiyo na kujionea Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Kieletroniki (eOPRAS) ambayo imetengenezwa na Wakala hiyo kupitia wataalam wa ndani.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, azma ya Serikali kuwasilisha Muswada Bungeni wa kubadili Wakala ya Serikali Mtandao kuwa Mamlaka ni kuwa na chombo thabiti kitakazowezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kufanya kazi kwa pamoja, kubana matumizi katika utengenezaji wa Mifumo ya TEHAMA kwa kutumia wataalam wa ndani na kuwezesha ukusanyaji wa mapato Serikalini.
Mkuchika ameongeza kuwa, Serikali imejiandaa na  inaendelea
kuwajengea uwezo wataalam wake wa TEHAMA nje ya nchi ili kuwa na hazina ya kutosha ya wataalam wabobevu katika eneo la TEHAMA.
Ameainisha kuwa, anajisikia fahari kushuhudia wataalam
wa ndani wakitengeneza Mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Kieletroniki (eOPRAS) ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika.

Sanjari na hayo, Mkuchika amedai kuridhishwa na utendaji kazi wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Maendeleo ya Mifumo ya Serikali Mtandao (eGOVRIDC) kilichojengwa na Serikali jijini Dodoma kwa ajili ya kuongeza kasi ya ukuaji wa Serikali Mtandao nchini.

Utekelezaji wa Serikali Mtandao (e-Government) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi 2019 umeongeza ufanisi katika utendaji kazi, umepunguza gharama za utendaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kwa urahisi, haraka na gharama nafuu.