Serikali kuwekeza kwenye miundombinu na huduma za mifugo

Na. Edward Kondela-Dar es Salaam 

Serikali imedhamiria kuwekeza zaidi katika miundombinu na huduma za mifugo ili Sekta ya Mifugo nchini iweze kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi, amebainisha hayo leo Julai 19, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati aliposhiriki katika mahojiano maalum na moja ya chombo cha habari nchini, ambapo amesema makusudio ya serikali ni kuifanya sekta hiyo kutoa mchango walau wa asilimia 10 kutoka asilimia saba ya sasa.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwenye minada ya mifugo tariban 51 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 17 ambapo lengo ni kuhakikisha mifugo inavunwa kwa wingi na kwenda kuzalisha nyama kwa ajili ya matumizi ya binadamu kwa kuongeza wigo wa masoko.” Amesema Prof. Mushi.

Aidha, amesema ongezeko la mauzo ya mifugo kwenye minada mwaka wa fedha 2021/22 nchi imerekodi mauzo ya Shilingi Trilioni 1.4 ilhali kwa mwaka wa fedha 2023/24 imerekodi mauzo ya Shilingi Trilioni 3.4 baada ya uwekezaji katika miundombinu ambapo mifugo inawekwa na kuuzwa.

Naibu Katibu Mkuu Prof. Mushi, ameelezea kuwa katika kipindi cha miaka mitatu nchi imeuza takriban Tani 40,000 za nyama nje ya nchi na kupata Shilingi Bilioni 435.

Amesema ili kuuza zaidi nyama nje ya nchi, serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo tayari majosho 746 yamejengwa katika kipindi kifupi ukiwa ni uwekezaji wa takriban Shilingi Bilioni 16 na kuhimiza wafugaji kuogesha mifugo yao ili kudhibiti magonjwa yanayosababishwa na kupe na mbung’o.

Ameongeza kuwa serikali imewekeza katika chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mifugo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 zimetumika dozi za chanjo Bilioni 1.1 ilhali kwa mwaka wa fedha 2023/24 zimetumika dozi Bilioni 1.4.

Kuhusu ufugaji wa kibiashara, amewataka wafugaji kubadilika na kufuga kisasa ili kuboresha hali zao za kiuchumi na kuwa na mtazamo wa kimasoko kwa kuwa na mifugo bora na yenye tija.

Pia, amewataka wafugaji kuzingatia lishe bora ya mifugo na kutumia chanjo kadri inavyoshauriwa na wataalamu badala ya kutumia virutubisho pekee vya kuongeza kinga kwa mifugo ili waweze kupata matokeo mazuri ya uzalishaji kwa mifugo yao.