Serikali yaandaa mwongozo wa kitaifa utoaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa
ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa kushirikishana uzoefu wa undeshaji wa
programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini jijini Dodoma
Wadau wa elimu wakifuatilia hotuba
ya Katika Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard
Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kushirikishana uzoefu
na uendeshaji wa Programu za mafunzo endelevu kwa walimu kazini jijini
Dodoma
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa
kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu ya mafunzo endelevu ya
walimu kazini wakifuatilia hotuba ya ufunguzi ya Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo
Katibu Mkuu wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya
pamojana wadau wa elimu baada ya kufungua mkutano wa wadau wa
kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya
walimu kazini.
……………………
Serikali imeaandaa mwongozo wa
Kitaifa wa utoaji wa Programu za Mafunzo Endelevu ya Walimu kazini
ambazo zitakwa na tija na pia kuongeza motisha kwa walimu.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard
Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kushirikishana uzoefu wa
uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Amesema pamoja na juhudi
zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha
elimu kumekuwepo na changamoto hivyo mwongozo huo utasaidia kuondoa
changamoto zinazojitokeza katika programu za mafunzo kazini kwa walimu
ikiwemo kutokuwa na mwendelezo na kukosekana kwa mfumo wa uratibu wa
uendeshaji wa mafunzo.
Dkt. Akwilapo amewataka wajumbe wa
mkutano kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni ili kuandaa miongozo ya
utekelezaji wa Programu za Mafunzo Endelevu ya walimu kazini nchini.
“Wizara ya Elimu imeona ni muhimu
kupata uzoefu kutoka kwa wadau na washirika wetu kutoka ndani na nje ya
nchi kuhusu namna Programu za Mafunzo endelevu ya walimu kazini
zinavyoendeshwa, naamini ushiriki wenu utasaidia kubaini maeneo muhimu
katika kuratibu kazi zilizobaki,” alisema Dkt Akwilapo
Katibu Mkuu Akwilapo aliongeza
kuwa kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikitekeleza programu za mafunzo
kazi kwa walimu ikiwepo Mpango wa Tanzania UNESCO na UNICEF (MTUU) na
Programu ya Kutegemeza Elimu ya Msingi Kiwilaya (DBSPE) hivyo uwepo wa
muongozo huo ni muendelezo juhudi hizo katika kuhakikisha mafunzo kazini
kwa walimu yanafanyika kwa ufanisi.
Nae Kamishna wa Elimu Dkt.
Lyabwene Mtahabwa amesema wazo la kuwa na muongozo kuhusu mafunzo
endelevu ya walimu kazini ni wazo ambalo nchi yoyote iliyo makini ambayo
inayotaka kuwa na walimu bora katika elimu inapaswa kuzingatia kwani
mafunzo ya awali ya walimu pasipo mafunzo endelevu kazini ni mafunzo
yasiyo kuwa na tija na kwamba vitu hivi viwili vinategemeana.
” Katika kipindi hiki tumeamua kwa
dhati kwamba baada ya mafunzo ya awali ya walimu watakapokwenda
kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi huko wakute wabobezi ambao
watawapokea na kuendeleza kuwapa utaalamu siku kwa siku ili waweze kukua
na kuendelea kitaalamu,” alisema Dkt. Mutahabwa
Kwa upande wake Msahauri wa Elimu
Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (DFID)John
Lusingu amesema uamuzi wa Serikali kuitisha kikao hicho cha wadau ni
jambo jema kwa kuwa wadau wanapata nafasi ya kuchangia katika kuboresha
badala ya mtu mmoja kuja na wazo na kutakiwa kufanyiwa kazi.
Mkutano wa wadau katika
kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya
walimu kazini unafanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 5, 2019 na
unashirikisha wadau mbalimbali kutoka Idara ya Maendeleo ya Kimataifa
DFID, Watafiti wa Elimu kutoka Marekani (RISE), EQUIP-T, Tusome Pamoja,
TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa wenyeji.