Serikali yafunga shule za awali hadi kidato cha sita kwa siku 30

Na.
Immaculate Makilika – MAELEZO
Kufuatia ugonjwa wa homa
ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) kuingia nchini, Serikali
imezifunga shule za awali hadi kidato cha sita kwa muda wa siku 30 kufuatia
kugundulika kwa mgonjwa wa Corona nchini.
Tamko hilo limetolewa leo
jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa wakati akitoa msimamo wa Serikali kuoitia vyombo vya habari kuhusiana
ugonjwa huo. 
 
 “Tumefunga shule zote kuanzia za awali hadi
kidato cha sita, tumesitisha michezo yote ikiwemo ligi kuu na Serikali imefikia
uamuzi huo ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini” alisema Waziri Mkuu.
 Image result for WAZIRI MKUU
Akitaja hatua mbalimbali
ambazo Serikali inaendelea kuchukua ni pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ambayo
si ya lazima kufanyika kama vile semina na shughuli mbalimbali za kijamii.
Aidha, Waziri Mkuu
Majaliwa, alisema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia abiria wanaoingia nchini
kupitia maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, kwa kuwapima abiria ili
kubaini kama wanamaambukizi, sambamba na kuimarisha maabara ili iweze kupima na
kutambua endapo kuna maambukizi.
“Tumetenga kambi maalum eneo
la Mloganzila jijini Dar es Salaam, kituo cha afya cha Buswelo huko Mwanza,
hospitali ya Mawenzi ya mkoani Kilimanjaro pamoja na hospitali za Mnazi mmoja,
Zanzibar na Chakechake huko Pemba, ambazo zitatumika kuhudumia wagonjwa wa
Corona” alisema Waziri Mkuu.
Sambamba na hilo, Waziri
Mkuu alisema kuwa jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kusitisha
shughuli za Mwenge na badala yake fedha hizo shilingi bilioni moja zimeelekezwa
Wizara ya Afya ili kuwezesha shughuli mbalimbali zitakazosaidia kupambana na
ugonjwa huo na tayari shilingi milioni 500 zimeshakabidhiwa Wizara ya Afya.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa
angalizo kwa Wizara ya Afya na wafanyabiashara na kusisitiza: “Wizara ya Afya
ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kuthibiti maambukizi (hand
sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na
Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa
viaa hivyo.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kufuatilia kwa
karibu na kufanya uchunguzi kuhusu wageni watakao ingia katika maeneo, na
wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika namba za bure za 0800110037/0800110124
na 0800110125 pindi watakapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ili
Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.
Ugonjwa wa Corona
ulioanza Disemba mwaka jana nchini China, umesambaa  zaidi katika nchi 150 duniani, na mgonjwa wa
kwanza kugundulika nchini  ni Machi 16
mwaka huu ambaye aliwasili nchini kutoka Ubelgiji.