Serikali yaguswa na juhudi za huawei kukuza tehama nchini

 

 

Group-photo-1024x593 Speaker-1024x475

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Dk.Jim Yonazi amepongeza juhudi za Huawei za
kuboresha ubora wa elimu ya ICT ili kuongeza ujuzi wa kuajiriwa kwa
wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Tanzania.

Dk Yonazi alitoa pongezi hizo wakati wa
Sherehe za Ufunguzi wa msimu wa tano wa programu ya “Seeds for the
Future” ambao ulifanyika mtandaoni mapema wiki hii.

Kwa mara ya kwanza hapa nchini, programu
ya “Seeds for the Future” ilizinduliwa mnamo 2016 kwa msaada wa Ofisi
ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Programu hiyo ilihusisha Vyuo Vikuu 4
wakati ikizinduliwa na sasa inajumuisha Vyuo Vikuu 7 ambavyo ni Chuo
Kikuu ya Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Taasisi ya
Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia
cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Agustino Tanzania (SAUT ) na Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam
(DUCE)

“Nimearifiwa kuwa katika kuchangia
ukuzaji wa vipaji vya TEHAMA nchini Tanzania na kuendana na mipango ya
kimkakati ya nchi, Huawei imeongeza kwa kiasi kikubwa shughuli na
ushirikiano na Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu hapa nchini. Hizi ni juhudi za
kupongezwa kwa kwa kuwawezesha vijana wa kitanzania. ” Dkt. Yonazi
wakati akitoa hotuba yake kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Zainab Chaula.

Pia, Dk Yonazi amewataka wanafunzi
kutumia maarifa wanayopata kwenye programu hiyo kufundisha wengine ili
kufaidisha idadi kubwa ya watu haswa wale ambao hawakuwa na bahati kama
wao.

“Nawapongeza wanafunzi wote ambao
wameshiriki katika program ya Seeds for the Future mwaka huu. Nawashauri
watumie fursa hii ipasavyo kukuza maarifa yao na kupata uzoefu wa
vitendo katika TEHAMA. Ninawahimiza pia kushiriki uzoefu waliopata na
wenzao ili kuendeleza na kunoa maarifa waliyoyapata.” Aliongeza

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa
Huawei Tanzania, Frank Zhou aliangazia mipango ya Huawei ya kuiwezesha
Tanzania kukabiliana na mahitaji ya teknolojia kidijiti ambayo
yanabadilika mara kwa mara.

“Tunafahamu kuwa maendeleo ya dijiti
yanahitaji mipango madhubuti ili kuiwezesha Tanzania kiuchumi kwa siku
zijazo. Katika zama hii mpya, ujuzi wa TEHAMA utakuwa muhimu kwa jamii,
kwa mashirika, na muhimu zaidi kwa vijana. Ndio maana tumewekeza kwa
kina katika mipango kadhaa haswa ukuzaji wa vipaji zna ujuzi.” Alisema.

Mwaka huu, ili kufikia vijana wengi zaidi
nchini Tanzania, Programu ya “Seeds for the Futrure” itafanyika
mtandaoni ili iweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi kutoka mikoa
tofauti na ili wanafunzi wenye mahitaji maalum pia washiriki.
Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, Huawei imeweza kuongeza idadi ya
nafasi za mafunzo kutoka wanafunzi 10 hadi 47.

“Ninajivunia kuwatangazia kwamba baadhi
ya washiriki hao ni wanawake, ambao wana nafasi muhimu sana katika
tasnia ya TEHAMA. Ninapenda kuhamasisha wanafunzi wengi wachanga
wanaohudhuria kozi hiyo kuangalia na kuijikita zaidi katika tasnia ya
Mawasiliano.” Aliongezea

Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na
Habari, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Leonard aliisifia program ya
“Seeds for the Future” na nafasi yake katika kuwawezesha vijana na
kukuza uwezo wa kuajiriwa.

“Programu hii ni mfano madhubuti wa
ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Huawei
Tanzania katika kujenga mazingira yenye afya na endelevu ya rasilimali
watu katika TEHAMA. Programu ya “Seeds for the Future” inafanya kazi
kama daraja ambalo linaunganisha pengo lililopo kati ya mafunzo ya
kinadharia na mahitaji ya vitendo katika soko la ajira. ”Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha
teknolojia wa Airtel, Bwana Prosper Mafole aliwahimiza wanafunzi kutumia
fursa za kujifunza zinazotolewa na Huawei na akawakaribisha kwa msaada
wowote endapo watahitaji.

Bwana Yuan Lin, Mshauri wa Uchumi na
Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, ameipongeza kampuni ya
Huawei kwa kuonesha mfano mzuri katika kukuza vipaji vya TEHAMA nchini
Tanzania kwa kuwajengea uwezo vijana wa shahada ya kwanza ambao watakuwa
msukumo wa mabadiliko ya TEHAMA nchini Tanzania katika siku za usoni.

“Ubalozi wa China nchini Tanzania
unahimiza makampuni mengine ya China kuwa na mipango kama hii ili
kusaidia katika kuandaa wataalamu ambao wanasimama imara katika
kutimiza malengo ya Tanzania ya uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya kipato
cha kati.” Alisema.

Sherehe ya ufunguzi wa “Seeds for the
Future” ilihudhuriwa na maafisa wa Serikali mashuhuri wakiwemo Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Mshauri wa Uchumi na
Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania Bwana Yuan Lin.