Serikali yakamata pombe kali imetelekezwa porini kukwepa kodi shinyanga

Serikali
mkoani Shinyanga imekamata pombe kali aina ya Shujaa, ambayo ilikuwa
imetelekezwa porini eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya
gari aina ya Roli lenye namba za usajili T 391 AES, kwa madai ya
kukwepa kulipa kodi.


Akitoa
taarifa kwa vyombo vya habari Novemba 9, 2019 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Zainab Telack akiwa kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga, eneo
ambalo gari hilo limewekwa chini ya ulinzi, amesema kuwa serikali
itawashughulikia wawekezaji wote ambao wanatabia ya kukwepa kulipa kodi
ya serikali.

Telack
ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa
Shinyanga, amesema Serikali inahitaji sana wawekezaji hapa nchini ili
kukuza uchumi wa taifa, lakini siyo wawekezaji wa kukwepa kodi na
kufanya biashara kiujanja ujanja.

“Pombe
hii kali ya Shujaa Katoni 1,490 tumeikamata ikiwa imefichwa porini eneo
la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya gari hili ambalo
mnaliona hapa, na wamiliki wa kiwanda hiki wamekuwa na tabia ya kukwepa
kulipa kodi na siyo mara ya kwanza kukamatwa,”amesema Telack.

“Hivyo
naagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Kesho wafike hapa, ili kufanya
tathmini ya kujua kiasi gani cha kodi ambacho watu hawa wanapaswa
kulipa, ili Serikali iweze kukusanya mapato na kupata fedha za
kutekeleza maendeleo kwa wananchi,”ameongeza.

Pia
ameonya baadhi ya Askari Polisi kushirikiana na waharifu hao wa kiwanda
cha Shujaa, na kuwapa mbinu za kukimbia ili kukwepa mkono wa Serikali,
na kumuagiza Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Shinyanga, kuwa ndani ya siku
nne, wamiliki wa kiwanda hicho wawe wameshakamatwa.

Kwa
upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Richard Abwao,
alithibitisha kukamata Pombe hiyo ya Shujaa, na kuahidi kutekeleza
maagizo hayo ya mkuu wa mkoa, huku akitoa wito kwa wamiliki hao wa
kiwanda cha Shujaa wajisalimishe wenyewe kwa usalama wao kwani
watakamatwa tu popote pale walipo.

Picha na Marco Maduhu- Malunde 1