Serikali yatoa maagizo kwa wamiliki viwanda vya chuma nchini

 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi, akitazama baadhi ya
malighafi katika kiwanda cha Fujian Hexingwang alipofanya ziara katika
viwanda hicho kilichopo Mkuranga na viongozi wa OSHA kwa lengo la
kufuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na serikali hivi karibuni
kuhusu uboreshaji wa mazingira ya kazi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi, akipitia nyaraka kuhusu
masuala ya Usalama na Afya katika kiwanda cha nondo cha Fujian
Hexingwang, alipofanya ziara katika kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.
Wanaomtazama ni Kaimu Mtedaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda na Meneja wa
Kanda ya Pwani wa OSHA, George Chali.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi (wa kwanza kushoto-kwa
waliovalia kofia zenye nembo ya OSHA), Kaimu Mtedaji Mkuu wa OSHA,
Khadija Mwenda, Meneja wa Kanda ya Pwani wa OSHA, George Chali na
Mkaguzi wa Usalama wa Umeme, James Bandoma, wakiwa katika picha ya
pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha nondo cha Fujian Hexingwang, wakati
viongozi hao walipofanya ziara katika kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi, akizungumza na
wafanyakazi wa kiwanda cha nondo cha Fujian Hexingwang, wakati kiongozi
huyo alipofanya ziara katika kiwanda hicho mwishoni mwa wiki akiwa
ameambatana na viongozi wa OSHA.

Na Mwandishi Wetu

Serikali imewaagiza wamiliki wa
viwanda vya chuma nchini kukaa kikao cha pamoja kwa ajili ya kujadili na
kukubaliana kuhusu teknolojia sahihi ya kuchambua vyuma chakavu ambayo
itakuwa na uwezo wa kutambua vitu vyenye milipuko wakati wa kufanya
uchakataji wa vyuma hivyo ili kutengeneza bidhaa mbali mbali za chuma.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi,
alipofanya ziara katika viwanda vya Fujian Hexingwang na Lodhia Group
of Companies vilivyopo Mkuranga kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa
maagizo ya kuboresha mazingira ya kazi yaliyotolewa na Wakala wa Usalama
na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) hivi karibuni.

“Wote wanaofanya bishara zinazohusiana
na kuchakata chuma wakae katika kikao cha pamoja watafute teknolojia
itakayo tusuaidia kugundua malighafi zenye mlipuko ili kuepuka ajali
zinasababishwa na uchambuzi usiofaa wa malighafi ya viwanda hivyo hali
ambavyo inasababisha kutokea ajali nyingi ambazo baadhi yake zimekuwa
zikigharimu uhai wa Watanzania wenzetu,” amesema Naibu Waziri Katabi.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija
Mwenda, ambaye aliambatana na Naibu Waziri katika ziara hiyo amesema
lengo la ziara hiyo ni kufuatilia maagizo ambayo yalitolewa na OSHA hivi
karibuni wakati Taasisi yake ilipokuwa ikichunguza ajali iliyotokea
katika kiwanda cha Fujian Hexingwang ambapo ajali hiyo ilisababisha vifo
vya wafanyakazi wawili.

Ameleza kuwa pamoja na wamiliki wa
kiwanda hicho kupewa maelekezo juu kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi
baada ya tukio la ajali kutokea na kugharimu maisha ya wafanyakazi
lakini bado kiwanda hicho hakijatekeleza kwa kiwango kikubwa.

“Tumekuja kuangalia utelezaji wa
maagizo tuliyoyatoa ili tufungue kiwanda hiki kiendelee na shughuli zake
lakini bado hawajatekeleza na sababu ya kutotekeleza tumebaini ni
kutokana na wenye kiwanda hiki kuwa na uelewa mdogo kuhusiana na mambo
tuliyowaelekeza. Hivyo, japokuwa kazi ya kutengeneza mifumo ya Usalama
na Afya mahali pa kazi ni wajibu wao lakini tumeamua kwamba tutaleta
watalaam wetu ili waweze kuwaongoza kwa karibu kusudi wakamilishe
marekebisho hayo muhimu na kisha tuwaruhusu kuendelea na uzalishaji,”
ameeleza Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA.

Aidha, amesema Taasisi yake kwasasa
inafanya ukaguzi wake kisekta kwa kuzingatia hali ya vihatarishi vya
kiusalama na afya (risk-based inspections) ambapo wamekwisha fanya
katika sekta kadhaa ikiwemo madini, fedha na hifadhi kwa jamii.

“Kwasasa tunaendelea na ukaguzi katika
viwanda vya chuma kote nchini. Baada ya kukamilisha ukaguzi huu na
kuandaa repoti tutazishirikisha mamlaki nyingine zikiwemo Wizara ya
Viwanda na Biashara pamoja ya Uwekezaji ili wanapoandaa sera, sheria na
miongozo mbali mbali ya uwekezaji wahakikishe kwamba miongoni mwa
matakwa muhimu kwa wawekezaji nchini ni kuwa na mifumo na teknolojia
sahihi zinazozingatia afya na usalama wa wafanyakazi,” alisema Mwenda.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija
Mwenda, ambaye aliambatana na Naibu Waziri katika ziara hiyo amesema
maagizo hayo waliyatoa hivi karibuni wakati Taasisi yake ilipokuwa
ikichunguza ajali iliyotokea katika kiwanda cha Fujian Hexingwang ambapo
ajali hiyo ilisababisha vifo vya wafanyakazi wawili.

Kwa upande wao wafanyakazi wa kiwanda
cha Fujian Hexingwang wameeleza kutofurashwa kwao na jinsi ambavyo
mwajiri wao anashindwa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria za
nchi.

“Haipendezi kuona mwekezaji kama huyu
anakiuka sheria na miongozo mbali mbali anayopewa na mamlaka mbali mbali
za serikali jambo ambalo linapelekea hata sisi wafanyakazi kukosa haki
zetu za msingi ikiwemo kufanya kazi katika mazingira salama,” alieleza
Ramadhani Mdimu.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri inafanyika
kwa lengo la kufuatilia maboresho yaliyofanyika kufuatia uchunguzi wa
ajali zilizotokea katika viwanda viwili vya chuma ambazo zinaonekana
zimetokea katika namna inayofanana. Aprili 17 na Mei 04 mwaka huu
zilirepotiwa ajali katika kiwanda cha PNP Industries Limited kilichopo
Mikocheni ambapo wafanyakazi watatu walijeruhiwa vibaya na nyingine
ilitokea katika kiwanda cha Fujian Hexingwang cha Mkuranga ambayo
ilipelekea vifo vya wafanyakazi wawili.