Serikali yawafichua watoto 16,000 wenye ulemavu waliofichwa na kuwaandikisha shule

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye
ulemavu, Mhe. Stella Ikupa amesema Serikali imewafichua na kuwatambua
jumla ya watoto 16,000 wenye ulemavu wa aina mbalimbali waliokuwa na
umri wa kwenda shule katika mikoa yote hapa nchini waliokuwa wamefichwa
na kuwaandikisha shule kulingana na mahitaji yao ya msingi.

Naibu waziri Ikupa ameyasema hayo Desemba 03, 2019 katika Maadhimisho ya
Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika
Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
“Watoto wenye mahitaji maalum waliokuwa wamefichwa Serikali imewatambua
na kuwaandikisha shule kulingana na mahitaji yao ya msingi, watoto
16,000 wametambuliwa kutoka mikoa na halmashauri zote nchini isipokuwa
Halmashauri tisa tu ambazo hazijafikiwa kwa kuwa zoezi hili ni endelevu
kadri bajeti itakavyoruhusu nazo zitafikiwa,”alisema Ikupa.
Aidha akijibu baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na  Shirikisho la
vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) kuhusiana na kutengewa bajeti 
ndogo amesema kuwa tayari serikali imetenga milioni 30 kwa ajili ya
kuliwezesha baraza la watu wenye ulemavu  kufanya kazi kwa ufanisi, huku
akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuongeza nguvu katika
kuwasaida watu wenye ulemavu hususani walio katika maeneo ya pembezoni.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri  Ikupa ametoa wito kwa vyama vya
siasa nchini kutenga nafasi maalum za uwakilishi bungeni kwa watu wenye
ulemavu kama kilivyofanya Chama Cha Mapinduzi( CCM), huku akiwasisitiza
wenye ulemavu na wao kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
badala ya kusubiri nafasi maalum pekee.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi
amesema Simiyu inawathamini na kuwajali watu wenye ulemavu huku
akibainisha kuwa Halmashauri zimetenga zaidi ya shilingi milioni 231
katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba
kwa watu wenye ulemavu na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo ili
wajikwamue kiuchumi.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bibi. Tungi Mwanjala ameiomba Serikali  
kuviwezesha viwanda vya ndani kutengeneza vifaa saidizi kwa watu wenye
ulemavu ili kupunguza gharama zitokanazo na kodi ya kuagiza vifaa hivyo
nje ya nchi.
Naye mmoja wa Watu wenye ulemavu Bi Nuru Awadh amesema katika kipindi
hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano watu wenye ulemavu wameaminiwa 
katika nafasi mbalimbali na sheria nyingi zinazowahusu watu wenye
ulemavu zitakelezwa kwa vitendo.
Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu mwaka 2019 yanaongozwa na
Kauli Mbiu inayosema: “HAMASISHA USHIRIKI WA WATU WENYE UELMAVU NA
UONGOZI WAO: TEKELEZA AGENDA ENDELEVU 2030”