Shirika la kuhifadhi misitu ya asili tanzania (tfcg lawanoa waandishi kuhusu habari za misitu mjini morogoro

Bw. Emmanuel Lyimo
kutoka Shirika la Utunziaji wa Misitu Tanzania (TFCG)akitoa mada katika
mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu habari za utunzaji wa misitu
inayofanyika kwenye hoteli ya Oacis mjini Morogoro kwa siku mbili.

Bi. Bettie Luwuge
kutoka shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCD) akitoa maelezo kwa
washiriki wa mafunzo ya uandishi wa habari utunzji wa misitu
inayofanyika mjini Morogoro.
 
Mwandishi Mkongwe wa habari Mwalimu Allan Lawa akitoa mada katika mafunzo hayo yanayofanyika mjini Morogoro.
Mwanasheria Wilson
Mukebezi akitoa mada kuhusu sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia
uhifadhi wa misitu wakati alipowasilisha mada katika mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada.
Bi. Bettie Luwuge kutoka shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCD) pamoja na baadhi ya watoa mada katika mafunzo hayo.
 
 
WAANDISHI wa habari 28 kutoka vyombo mbalimbali vya habari wamepatiwa mafunzo na kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM).
 
Mafunzo hayo
yametolewa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao
wa Jamii wa Usimamizi Misitu Tanzania (Mjumita), Shirika la Kuendeleza
Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) ambayo yanatekeleza Mradi wa Kuleta
Mageuzi Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), chini ya ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la Uswis (SDC).
 
Akizungumzia lengo
la mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema
mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu
rasilimali misitu inavyoweza kutunzwa na kutumika kwa faida ya jamii
husika.
 
Lyimo alisema
waandishi wa habari in kiungo muhimu kati ya jamii na watunga sera hivyo
wao wanaamini kundi hilo likipata uelewa litarahisisha jamii nzima
kuelewa lengo lao.
 
“Tumekuwa na
utekelezaji wa mradi wa TTCS kwa takribani miaka saba sasa hivyo wakati
tunatekeleza mradi kwa wananchi waandishi wa habari ndio kiungo sahihi
ya kufikisha ujumbe kwa jamii bila kupindapinda,” alisema.
 
Lyimo alisema
wamekuwa wakishirikisha waandishi wa habari kila mara ili kuhakikisha
kunakuwepo kizazi ambacho kitadumu kwenye uandishi wa aina hiyo kila
wakati.
 
Alisema walilazimika
kuja na mradi huo ili kuhakikisha misitu ya vijiji inakuwa salama na
endelevu jambo ambalo limeweza kuonekana kivitendo.
 
Lyimo alisema mradi
wa mkaa endelevu umeweza kufanya mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa
wananchi wengi vijijini hivyo waandishi wa habari wakielewa wataweza
kufukisha ujumbe kwa haraka.
 
Alisema misitu ni
rasilimali ambayo inaweza kukabiliana na changamoto zilizopo kwa jamii
hivyo wamekuwa wakijengea uelewa wanavijiji kuhusu faida za matumizi
endelevu ya rasilimali hiyo.
 
Aidha, Lyimo alisema utafiti umeonesha kuwa misitu mingi inamalizika kutokana na uanzishaji wa mashamba mapya.
 
Alisema kilimo
pamoja na umuhimu wake kwa jamii kimekiwa kikichangia upotevu wa misitu
kuliko ukataji wa mkaa hivyo ni jukumu la vyombo vya habari kuonesha
hali halisi.
 
“Tumetembelea wilaya
67 mikoa 22 matokeo yanaonesha ukataji wa misitu unasababishwa na
uandaaji wa mashamba mapya na mkaa ni sehemu ndogo hali ambayo
inachangia upotevu wa hekta 469, 000 kila mwaka,” alisema.
 
Mkurugenzi huyo
alisema ili  changamoto hiyo ifahamike kwa jamii na watunga sera
waandishi ndio kiungo sahihi hivyo ni imani yake mafanikio yatapatikana.
 
Ofisa Wakujengea
Uwezo wa TFCG, Simon Lugazo alisema mradi huo umeweza kuchochea
mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na maendeleo kwenye vijaji vya
mradi.
 
Lugazo alisema hadi
sasa vijiji,halmashauri na wanavijiii wamefanikiwa kuingiza zaidi ya
Sh.Bil 3 ambazo zimefanikiwa kitekeleza miradi ya maendeleo.
 
Alisema fedha hizo zimeweza kutekeleza miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na uhifadhi wa misitu ukiimarika.
 
Ofisa Uhusiano wa
TFCG, Bettie Luwuge aliwataka waandishi kutembelea vijiji ambavyo
vinatekeleza miradi ya uhifadhi ili kujionea.
 
“Tumekuwa
tukisisitiza USM katika vijiji na matokeo chanya yameonekana tunapaswa
kueleza jamii faida na hasara ambazo zinaonekana huko,” alisema.
 
Kwa upande wake
Mwandishi wa Habari Mkongwe, Allan Lawa amewataka waandishi wa habari
kuwa wabunifu kwa kuandika habari ambazo zinagusa jamii na nchi kwa
ujumla.
 
Lawa alisema iwapo
waandishi wa habari watatumia kalamu zao kwa ufasaha watakuwa na mchango
mkubwa kwenye sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.