Simbachawene agoma kufungua machinjio ya msalato jijini dodoma

Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George
Simbachawene hii leo amegoma kufungua machinjio ya Msalato jijini Dodoma
kwa kutokidhi vigezo vya ubora vinavyoridhisha ikiwemo ukarabati wa
kiwango cha chini na kutoa muda wa wiki ya moja kurekebisha dosari
zilizobainika.

 
Ametoa
uamuzi huo wakati akitembelea jengo la machinjio ya Msalato jijini
Dodoma wakati wa ziara aliyoifanya na kubaini kasoro mbalimbali
zinazotakiwa kupatiwa ufumbuzi. “Sifungui hii machinjio kwa sababu
hamjajiandaa na ujenzi uko hovyo kwahiyo siwezi kufungua kitu cha hovyo
namna hii” Simbachawene alisisitiza.
 
Akiongea
katika ziara hiyo amesema amesikitishwa sana na ukarabati wa
kurekebisha machinjio hayo kwani haukidhi viwango na ujenzi wake ni wa
kiwango cha chini hivyo amemuagiza Afisa Mipango Miji wa Jiji la Dodoma
Bwana Shabani Juma kuhakikisha ndani ya wiki ya moja kila kitu
alichotolea maelekezo kifanyiwe marekebisho.
 
“Sijafurahishwa
kwa kwakweli, majengo ya Serikali yanatakiwa kujengwa na mafundi
classic, vitu vya Serikali viwe State of Art” Simbachawene alisisitiza.
 
Waziri
Simbachene pia amegiza kuandaliwa kwa taarifa rasmi ya ukarabati huo
ikiwa ni pamoja na thamani ya fedha zilizotumika katika zoezi zima la
ukarabati na ujenzi wa  mifumo ya maji safi na maji taka.
 
Naye
Diwani wa Kata ya Msalato Mheshimwa. Ali Mohamed amesema kuwa
amesikitishwa sana kwa kutofunguliwa kwa machinjio hiyo kwani wakazi
wengi wa Kata yake wanategemea machinjio kwa shughuli zao za kila siku
kwa sababu ni Wafugaji. Pia alisema Maelekezo yote yaliyotolewa na
Mheshiwa Waziri Simbachawene wameyapokea na naamini kuwa yatarekebishwa
kwa wakati.
 
Machinjio
hiyo ya Msalato ilifungwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimazi wa
Mazingira (NEMC) tarehe 31 Oktoba 2019 kutokana na sababu za mazingira
yasiyokua safi na salama, kufuatia ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Viwanda, Biashara na Mazingira.