Spika ndugai asema mbowe ni mtoro bungeni

Spika
wa Bunge, Job Ndugai amesema utoro wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe umekuwa ukisababisha nafasi ya maswali
ya moja kwa moja kutoka upinzani kwenda kwa Waziri Mkuu kupotea kila
mara.


Ameyasema hayo jana Novemba14,2019  bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu kutoka kwa Wabunge.

Ndugai
alisema kwa mujibu wa utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola
Upinzani hupewa nafasi ya kwanza kuiuliza swali Serikali, lakini kwaa
hapa nchini nafasi hiyo hupotea kila wakati kutokana na utoro wa
kiongozi huyo.

“Waheshimiwa
Wabunge niwataarifu tu kwamba utaratibu wetu wa kipindi cha maswali kwa
Waziri Mkuu swali la kwanza kabisa huwa linakuwa hakiba kwa kiongozi wa
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, lakini kwa leo kama mnavyoona kiongozi
huyo hayupo,” alisema Spika Ndugai.

Alisema
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani anaweza siku zote asiwepo bungeni
lakini siku ya Alhamisi ni muhimu awepo kutokana Waziri Mkuu kuwapo na
anatakiwa awe wa kwanza kuuliza swali.

“Huwa
ni fursa pekee ambayo upinzani wanapata nafasi kwa hiyo kiongozi wa
upinzani anaweza asiwepo bungeni siku yoyote lakini siku ya alhamisi
ambayo ni ya maswali kwa Waziri Mkuu ni lazima awepo,” alisema Spika
Ndugai

Alisema hata hivyo hana taarifa zozote za udhuru kutoka kwa kiongozi huyo (Mbowe) na wala hajui yuko wapi.

“Kwa
hiyo hatujapata swali lile kwa kuwa kiongozi wa upinzani bungeni
hayupo, uwe wapi, uwe wapi kama Spika hana taarifa zako ni mtoro tu kwa
hiyo, ni mtoro na ndiyo maana leo unaona kwamba hiyo fursa ambayo
imewekwa kwenye kanuni haijaweza kutekelezwa.

“Na ndio maana mnaona kwamba nafasi inapotea potea sababu ya utoro,”alisema Spika Ndugai.