Taarifa kwa umma toka wakala wa huduma za misitu tanzania (tfs)

Wakala
wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatoa wito kwa umma kuchukua
tahadhari na matumizi ya moto kwenye maeneo yanayokaribiana na misitu.
Tunawaomba wananchi wote wakiwemo wavunaji, warina asali, wawindaji,
wafugaji na hususani wakulima kuepuka matumizi ya moto katika kuandaa
mashamba kwani wamekuwa ni chanzo kikuu cha moto unaoingia kwenye misitu
hasa kunapokuwa na upepo mkali.

Tunapenda kuuarifu umma kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na
ongezeko la matukio ya moto katika mikoa ya Iringa na Njombe
iliyopelekea kuunguza mashamba ya miti ya watu binafsi na yale ya
serikali hususani shamba la miti la Sao Hill lililopo katika wilaya ya
Mufindi. Moto huo umeunguza sehemu tofauti za msitu huo na kusababisha
hasara kufuatia kuungua miti ya umri tofauti.
TFS inapenda kutoa pole kwa wadau waliounguliwa vifaa vyao vya uvunaji
pamoja na mazao yaliyovunwa wakati mashine ya kuangushia miti (chainsaw)
ilipolipuka ghafla katika moja ya tukio lililopelekea kusambaa kwa
moto. 
Aidha, tunatoa shukrani nyingi sana kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama (W)
Mufindi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), JKT Mafinga, Jeshi la
zimamoto, Jeshi la Akiba, wavunaji wa shamba la Sao Hill, vikosi vya
moto vya shamba, watumishi wa TFS na wananchi wote wa maeneo jirani kwa
ushirikiano wao wa hali na mali katika kupambana na moto. 
Katika hatua hiyo ninawakumbusha tena kwa mara nyingine waandaaji wa
mashamba kuhakikisha kuwa wanapata vibali vya matumizi ya moto kwa
mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 kama sehemu ya
kukabiliana na changamoto hii.
Tunatoa wito kwa wananchi wote kuepuka shughuli zozote ambazo zinaweza
kupelekea au kusababisha moto kwenye misitu ya asili au ya kupanda kwani
moto ni adui namba moja wa misitu yetu.
Imetolewa na
Prof Dos Santos Silayo
KAMISHNA MHIFADHI – TFS