Taasisi ya usuluhishi yaomba mabadiliko ya sheria

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wajumbe kutoka Taasisi ya Usuluhishi
Tanzania walipofika kumtembele ofisini kwake jijini Dar es salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka
Taasisi ya Usuluhishi Tanzania walipofika kumtembele ofisini kwake
jijini Dar es salaam.
Na Lydia Churi-Mahakama
Taasisi ya Usuluhishi Tanzania
(The Tanzania Institute of Arbitrators) imeiomba Mahakama ya Tanzania
kusaidia katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi ya mwaka
1931 (The Tanzania Arbitration Act, 1931) kwa kuwa sheria hiyo hivi sasa
imepitwa na wakati. 
Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931
ilifanyiwa marekebisho (Amendment) mara moja tangu Tanzania ipate Uhuru
wake ambapo marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1971. 
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Gabriel
Malata alitoa ombi hilo leo wakati ujumbe kutoka Taasisi hiyo
ulipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ofisini kwake kwa lengo la kujenga mahusiano ya kiutendaji kati yake na
Mahakama ya Tanzania na pia kutambulisha uongozi mpya wa Taasisi hiyo.
Akizungumzia mchakato wa
mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi, Bwana Malata aliiomba Mahakama
kuishirikisha Taasisi hiyo kwa karibu katika mchakato wa mabadiliko ya
Sheria ya Usuluhishi na hususan katika hatua ya utengenezaji wa kanuni.
Alisema Taasisi ya Usuluhishi
Tanzania iko tayari kutoa maoni na mapendekezo pindi hatua hiyo
itakapofikiwa. Aliongeza kuwa hivi sasa Taasisi hiyo imejikita katika
kutoa Elimu husika katika Shule ya Sheria (Law School of Tanzania)
ambapo wanafanya vipindi ili waweze kupata Wasuluhishi bora hapo
baadaye.
Mwenyekiti huyo alisema Taasisi
yake inao mfumo unaowatambua Wasuluhishi hai na hivyo ameiomba Mahakama
kuishirikisha ili wapatikane wasuluhishi hai. Sheria ya Tanzania
inaruhusu kuteua Wasuluhishi.
Kwa Upande wake, Jaji Mkuu wa
Tanzania amesema Mahakama iko tayari kurekebisha Kanuni za Usuluhishi
pale inapobidi kufanya hivyo ili Tasnia ya usuluhishi ifanye kazi vizuri
na kuwasaidia wananchi kwa haraka.
Alisema suala la usuluhishi ni muhimu kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa litasaidia kupunguza idadi ya kesi mahakamani.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, utafiti
unaonyesha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama linaweza
kufanyika katika ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo
mpaka Mahakama ya juu. 
Aidha, Jaji Mkuu ameishauri
Taasisi ya Usuluhishi Tanzania kuhakikisha inatoa zaidi elimu juu ya
masuala ya usuluhishi kwa kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa wa
masuala hayo.