Taasisi zote za Serikali zapewa Miezi sita kujiunga mfumo wa Serikali Mtandao (e-GA).

Na, Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.

Taasisi zote za umma zimepewa muda wa miezi sita(6) kuhakikisha zinakuwa katika mfumo wa pamoja wa Serikali Mtandao utakaosaidia kusomana na kurahisisha utendaji kazi.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao kazi cha tano cha Serikali Mtandao kinachoendelea Jijini Arusha, Makamu wa Rais Dkt. Philp Mpango amesema kufikia muda huo aliotaja mikoa miwili ambayo haijajiunga na mfumo kuhakikisha inatekeleza agizo mara moja.

Dkt. Mpango ameeleza kuwa katika ukomavu wa matumizi ya Teknolojia Duniani katika utoaji wa huduma za serikalini, ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index), katika nchi 198 duniani ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Machi 2023 ilibainisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A, na kushika nafasi ya 26 Duniani, nafasi ya 2 Barani Afrika baada ya Mauritius na nafasi ya 1 Afrika Mashariki kwenye ukomavu wa matumizi ya (TEHAMA) Serikalini.

“Kipekee napongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali mtandao (e-GA) , hatua hii imeokoa muda, pesa na kurahisisha huduma kwa wananchi, lakini pia nawahimiza kushirikiana na TCRA na Vyombo vya Dola ili kudhibiti vitendo vya uhalifu mtandaoni, katika hayo yote taasisi zote za umma ziainishe na kuuhisha taarifa zake kwa lengo la kubadilishana taarifa” amefafanua Dkt. Mpango.

Ametaja kuwa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza katika jitihada mbalimbali za kuendeleza na kuboresha Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) dhamira kuu ikiwa ni kuhakikisha serikali inaendesha shughuli zake kidigitali na kuwapatia wananchi huduma kwa bei nafuu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema jukumu la kuboresha utendaji wa serikali ni kurahisisha huduma kwa wananchi.

“Serikali mtandao (e-GA) ni kiungo muhimu kinachosaidia wananchi kupata huduma rahisi na bila ya rushwa, kama Kiongozi wenu naridhishwa na utendaji kazi wenu ambao umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi na kuharakisha maamuzi” amesema Simbachawene.

Hata hivyo ametaja mafanikio ya mamlaka yaliyofikiwa kuwa ni kuunganishwa kwa mifumo 218 kutoka taasisi 181 ambazo tayari zimeanza kubadillishana taarifa, na kubainisha kuwa jitihada za kuunganisha mifumo mingine zinaendelea.

Katika namna hiyohiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema Serikali Mtandao (e-GA) ilianzishwa kupitia sheria ya serikali mtandao ya mwaka 2019 na kupewa jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za serikali mtandao pamoja na kusimamia uzingatiaji wa sera, sheria na kanuni na miongozo ya serikali mtandao katika taasisi za umma.

“Mafanikio tuliyofikia tangu kuanzishwa kwa mamlaka hii ni ujenzi wa matumizi Rasilimali shirikishi za (TEHAMA) ukiwemo mfumo wa Barua pepe Serikalini (GMS) unaotumiwa na taasisi 770, mfumo wa huduma za serikali kupitia simu za mkononi (m Gov) unaotumiwa na taasisi 429, mfumo wa ofisi mtandao (GeOS) unaotumiwa na taasisi 347 pamoja na Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GovNet) ambao umeunganishwa na ofisi 457 za umma”,

“Mafanikio mengine ni ujenzi wa mifumo tumizi ya Kisekta na Kitaasisi kwa kushirikiana na taasisi husika ikiwemo mfumo wa kusimamia Rasilimali watu serikalini (New HCMIS) uliojengwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambao unatumiwa na taasisi 466 kati ya taasisi 530” amesema Mhandisi Ndomba.