Tahadhari ya mvua kubwa na upepo kwa siku 5

Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya mvua kubwa na upepo
mkali katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam,
Zanzibar na Pwani kwa muda wa siku tano kuanzia jana.


Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kuanzia jana hadi Jumapili,
kunatarajiwa kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa kwa baadhi ya maeneo
ya Pwani ya Bahari ya Hindi, hivyo kusababisha shida kwenye uvuvi na
usafiri wa baharini.

“Kiwango cha mvua na upepo ni cha wastani, hivyo wananchi wachukue
tahadhari katika shughuli zao,” TMA ilieleza katika taarifa yake hiyo.

Ilisema athari huenda zikajitokeza kutokana na kusimama kwa shughuli za
binadamu, kuharibika kwa miundombinu na makazi kuzingirwa na maji, hivyo
kuna haja kuchukua tahadhari.

Mamlaka hiyo ilisema mvua inayonyesha sasa ni mwendelezo wa utabiri wa
mvua za vuli ilioutoa kipindi cha nyuma na katika baadhi ya maeneo
itaendelea hadi mwezi ujao.