Takukuru mwanza yaokoa na kudhibiti upotevu wa zaidi ya sh. milioni 50

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa
wa Mwanza, Emmanuel Stenga, akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi
hiyo kwa waandishi wa habari jana, katika kipindi cha Julai-Septemba
mwaka huu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa
wa Mwanza, Emmanuel Stenga, akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa
habari jana,yaliyolenga utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha
Julai-Septemba mwaka huu.


Waandishi wa habari
baadhi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza
Emmanuel Stenga (mwenye tai nyekundu) wakiwemo watumishi wa taasisi hiyo
jana.

Picha na Baltazar Mashaka


…………………………..

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA 
 


TAASISI ya Kupamba na Kuzuia
Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imeokoa na kudhibiti upotevu wa fedha
zaidi ya sh. milioni 50 mkoani humu huku kati ya fedha sh. milioni 30
zikirejeshwa kwenye akaunti maalumu ya serikali.


Akizungumza na waandishi wa habari
jana Mkuu wa TAKUKURU mkoani humu Emmanuel Stenga alisema kuwa uokoaji
na udhibiti wa upotevu wa fedha hizo ulifanyika katika kipindi cha
Julai-Septemba mwaka huu. 


“TAKUKURU Mkoa wa Mwanza katika
mapambano ya rushwa, udhibiti wa ubadhirifu wa fedha za umma kwa kipindi
cha Julai hadi Septemba, 2019 imefanikiwa kuokoa sh.42,529,840 na
kudhibiti upotevu wa sh.8,294,560.Kati ya fedha hizo sh.30,206,840
zemerejeshwa BOT kwenye akaunti maalumu ya serikali,’alisema Stenga.


Alisema kiasi kingine cha
sh.11,413,000 zilizobainika kufanyiwa ubadhirifu kwenye mradi wa ujenzi
wa zahanati ya Kijiji cha Salongwe wilayani Magu pia kimerejeshwa kwenye
akaunti ya serikali ya kijiji hicho.


Pia Stenga alisema, sh. 640,000
zimerejeshwa baada ya ukaguzi wa taasisi hiyo kufanyika kwenye mradi wa
ujenzi wa Shule ya Msingi Kakerege wilayani Ukerewe baada ya kubainika
kuwa madirisha yaliyowekwa kwenye vyoo vya shule hiyo kutolingana na
thamani ya fedha iliyolipwa.


Aidha, taasisi hiyo ilikagua
miradi nane ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya yenye
thamani ya sh.2,152,600,000 ili kuona fedha za serikali zinatumika kwa
usahihi na miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na
thamani ya fedha.
 

Stenga alifafanua kuwa kati ya
miradi iliyokaguliwa sita ni yelimu yenye thamani ya sh. milioni 806.6,
maji mradi mmoja wenye thamani ya milioni 986 na afya wenye thamani ya
sh. milioni 360 na walifuatilia na kukagua fedha za ruzuku zinazotolewa
na serikali kwa shule za msingi ambapo 70 zilikaguliwa katika
halmashauri  zote za Mkoa wa Mwanza.
 

“Lengo kuu la ufuatiliaji huu
kwenye miradi inayotekelezwa, ni kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wa
rasilimali ama kudhibiti fedha za serikali inapobidi katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali ili itekelezwe kwa kiwango kinachotakiwa na thamani
ya fedha ionekane,”alisema Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani humu