Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga kupitia dawati la uchunguzi kwa kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 imepokea taarifa 19 za malalamiko ambapo taarifa zinazohusu Rushwa ni 13 na kwamba uchunguzi wake unaendelea huku taarifa zisizohusu Rushwa ni sita (6).
Akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amefafanua kuwa taarifa hizo za malalamiko zimetokea sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi taarifa mbili (2), Maji taarifa mbili (2), Elimu taarifa mbili (2), Kilimo taarifa moja, Nishati taarifa moja, Madini taarifa moja, Mahakama taarifa moja, Polisi taarifa moja, Afya taarifa moja na Ardhi taarifa moja ambapo amesema uchunguzi wa taarifa hizo bado unaendelea.
Ameongeza kuwa taarifa zisizohusu Rushwa watoa taarifa wake walishauriwa mahala sahihi pa kupeleka taarifa zao na kwamba taarifa nyingine zilifungwa baada ya kufanyiwa kazi ikiwemo taarifa zinazohusu sekta ya Ardhi mbili (2), Elimu moja, Ajira moja, na Mahakama moja.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ametaja kesi zinazoendelea Mahakamani huku akieleza mikakati ya utendaji kazi kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Machi Mwaka huu 2024.
“Kesi zinazoendelea Mahakamani kwa kipindi hiki ni tisa (9), kesi mpya nne (4) na kati ya hizo kesi mbili ziliamuliwa na Mahakama moja tulipata ushindi na moja ilishindwa, kesi iliyoshinda ni kesi (CC 25/2023) mshtakiwa aliamuliwa kulipa faini ya Shilingi 200,000 au kwenda jela kifungo cha Miaka miwili na mshtakiwa alilipa faini, pia Mahakama iliamuru mshtakiwa kurejesha kiasi cha Shilingi 200,000 alizojipatia kwa njia ya Rushwa kwenye akaunti ya jumuiya ya watumiaji Maji (CBWOS) Bubiki”. amesema Kessy
“Kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Machi Mwaka huu 2024, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga tutajikita zaidi kwenye ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha kama serikali ilivyokusudia pia kufanya warsha na kusimamia utekelezaji wa maazimio yote ya changamoto mbalimbali zilizobainika kwenye chambuzi za mifumo na miradi ya maendeleo”.amesema Kessy
Aidha mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amefafanua zaidi kuwa taasisi hiyo katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ilifanya ufuatiliaji wa miradi ya SEQUIP (mpango wa uboreshaji wa Elimu ya Sekondari) ili kuona hali ya utekelezaji wa miradi kwamba inatekelezwa kwa wakati na katika ubora na viwango vinavyotakiwa.
“Kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 Mkoa wa Shinyanga ulipokea jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 5.2 (5,283,343,372) Fedha hizi zilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi 13 ambayo ni Shule mpya sita (6) za Sekondari, ujenzi wa Nyumba sita 2 in 1 za Walimu na ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa”.
“Pia TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga iliweza kufanya ufuatiliaji wa miradi kumi (10) ya SEQUIP yenye thamani ya Shilingi 4,063,343,372 na kujiridhisha kuwa mbali na uwepo wa changamoto zinazorekebishika, miradi hiyo imetekelezwa kwa ufanisi na ubora unaotakiwa na miradi hiyo kama Shule na Nyumba za Walimu imeshaanza kutumika”.
“Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inatoa wito kwa wananchi kushiriki zaidi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo kwani baadhi ya utekelezaji wa miradi hii ya SEQUIP imeshirikisha jamii hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa miradi hii kutekelezwa kwa ufanisi”.
Pia ametaja miradi mingine miwili ya maendeleo iliyofuatiliwa ambayo inatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala yenye thamani ya Shilingi Milioni mia saba (700,000,000) ambapo dosari ndogo ndogo zilibainika ikiwemo ujenzi wa kituo cha Afya Bulige Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
“Dosari ndogo ndogo zilibainika kwenye miradi na ushauri ulitolewa kwa kutatua dosari hizo katika ujenzi wa kituo cha Afya Bulige Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imebainika kuwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Shilingi 25,000,000 yakiwemo Madirisha ya Alluminium vimelipiwa lakini vifaa hivyo havijafikiwa kwenye eneo la mradi na havipo kwenye kumbukumbu ya vitabu vya stoo hatua iliyochukuliwa tumeanzisha uchunguzi”.amesema Kessy
Amesema taasisi hiyo ilifanya chambuzi tano (5) za mfumo katika mfumo wa matumizi ya Fedha za TASAF, utoaji wa huduma katika sekta ya Ardhi kupitia mabaraza ya Ardhi na Nyumba, matumizi ya stakabidhi za EFD kwa wazabuni wanaofanya biashara na Halmashauri katika Halmashauri ya Kahama, Shinyanga na Kishapu.
“Katika uchambuzi wa mfumo kuhusiana na stakabadhi za EFD kwa wazabuni wanaofanya biashara na Halmashauri TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga tulibaini kuwepo kwa risiti za EFD ambazo ni za kughushi lakini pia tulibaini kuwepo kwa EFD zenye utambulisho wa TIN namba ya mfanya biashara tofauti na anaye toa huduma au bidhaa lakini tumeshauri elimu zaidi itolewe kwa wananchi dhidi ya matumizi sahihi ya risiti za EFD na kuanzishwa kwa uchunguzi wa risiti za kughushi”.
“Katika uchambuzi wa mfumo kuhusiana na utoaji wa huduma za Ardhi kupitia mabaraza ya Ardhi ilibainika wananchi kutokulipa kodi ya pango la Ardhi na Nyumba baada ya mwananchi kufanyiwa umilikishaji tulichukua hatua za kushauri elimu zaidi itolewe kwa wananchi juu ya matakwa ya sheria yanayopaswa kufuatwa ili mwananchi aweze kumiliki Ardhi kisheria na majukumu yake baada ya kummilikisha”.
“Ucheleweshwaji wa kutatua migogoro ya Ardhi kwenye mabaraza ya Ardhi pia wananchi kukosa elimu juu ya sheria ya Ardhi ya namna ya kupata hati miliki na kutatua migogoro ya Ardhi endapo ikitokea”.
“Utunzaji wa hafifu wa taarifa za umiliki wa viwanja pamoja na taarifa mbalimbali za wateja tumeshauri serikali kutumia njia ya kidijitali katika kutunza taarifa zote za ummiliki wa viwanja ili kuendana na mabadiliko ya tekinolojia”.
“Katika uchambuzi wa mfumo wa matumizi ya Fedha za TASAF ilibainika kuna madai ya wasimamizi wa miradi na mafundi ambayo hajalipwa tumemtaka mratibu wa TASAF Mkoa wa Shinyanga kufanya mawasiliano na TASAF makao makuu ili madai hayo yalipwe kwa wahusika”.amesema Kessy
Mkuu huyo amesema ofisi imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Elimu ya masuala ya Rushwa inatolewa katika taasisi za Serikali, binafsi na wananchi ili kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya Rushwa.
TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano kwa Serikali kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa ubora.
“Kama mwananchi yoyote ataona kuna vitendo ambavyo vinaashiria ubadhilifu wa Fedha za miradi hiyo atoe taarifa TAKUKURU, kwa ofisi zetu zilizopo mtaa wa Uzunguni mkabala na Nyumba za bodi ya Pamba au piga simu namba 0738-150196 au 0738-150197, ofisi ya Kahama simu 0738-150198 na ofisi ya Kishapu simu 0738-150199 au piga simu bure 113”.