Takukuru yatahadharisha rushwa kuelekea uchaguzi mkuu 2020..”atakayebainika na rushwa ataonja jiwe la joto…”

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU,Brigedia Jenerali John Mbungo amewatahadharisha wanasiasa wa nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Udiwani na Ubunge kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kampeni za uchaguzi kwani atakayebainika ataonja joto la jiwe.


Brigedia Jenerali Mbungo ametoa rai hiyo hii  Juni 17,2020 Ofisini kwake Makao Makuu ya TAKUKURU Jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba Mwaka huu.

Amebainisha kuwa ni vyema sasa  kwa wagombea  na watia nia ambao wanatarajia kuwania nafasi hizo mblimbali za uongozi kujitathmini kwa kina na kuona  kama wanafaa kuwa Viongozi na kama hawafai ni bora waache kuliko kuingia na kuanza kuwarubuni Wapiga kura kwa kuwapa hongo ya vitu mbalimbali ikiwemo fedha pamoja na Chakula ambapo amesema wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha amesema kuwa katika kuelekea uchaguzi Mkuu Taasisi yake imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitaka nafasi za uongozi jambo ambalo ni kinyume na Sheria za Uchaguzi.

Pia amewaonya wananchi kuacha kujiingiza  katika  vitendo  vya rushwa kwakudhani kuwa mchakato huo wa uchaguzi ni wa mavuno kwao kwa kujipatia chochote kwa njia ya rushwa.

Mkurugenzi huyo wa TAKUKURU ametaja madhara ya rushwa ni pamoja na kudumaza demokrasia,kuwa na viongozi wasiowajibika.

Uchaguzi Mkuu wa Madiwani na Wabunge unatarajiwa kufanyika Oktoba25 Mwaka huu.

MWISHO