na Kenya zimeahidi kuendeleza na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa
maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 56 ya Jamhuri ya Kenya, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu na nchi hizo
zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya diplomasia
ya uchumi baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
“Sisi Tanzania na Kenya ni ndugu wa damu, kwa hiyo basi tunawatakia sana
kila la kheri katika kuiletea Kenya maendeleo…lakini mjue kuwa
maendeleo ya Kenya ni maendeleo ya pia ya Tanzania, maendeleo pia ya
Uganda, ni maendeleo pia Burundi, maendeleo pia Rwanda na Maendeleo pia
ya Sudani Kusini na ni maendeleo pia ya jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu
ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa
ikionesha kwa Kenya na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya
maendeleo kwa Tanzania na Kenya.
“Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya
maendeleo baina ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu
na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu
ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu”.
Alisema Balozi Kazungu.
Aidha, Balozi Kazungu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya
kipekee kwa taifa la Kenya kutokana na mshikamano ambao imekuwa
ikionesha kwa nchi ya Kenya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili 2019 Kenya tulipokutana na Tanzania
jijini Arusha tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara 25 kati ya 37, hii
inadhihirisha ni kwa jinsi gani Kenya na Tanzania na ndugu ambao
wanapenda kukuza na kuendeleza maendeleo ya biashara”. Ameongeza Balozi
Kazungu.