Tanzania kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini israel

Tanzania
inatarajia kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini Israel ambao
wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii
mwezi huu wa Oktoba.


Kundi la kwanza lililokuwa na zaidi ya watalii 200 liliwasili nchini
kuanzia tarehe 05 Oktoba na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520
linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 na kundi la tatu lenye watalii
zaidi ya 200 litawasili nchini tarehe 13 Oktoba kupitia Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Watalii wengine zaidi wanatarajiwa
kuwasili nchini mwezi huu baada ya Makampuni ya Uwakala wa Utalii
kukamilisha taratibu za safari zao.
Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za
Taifa za Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ujio
wa watalii hao unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa
utalii  wa ndani na nje ya nchi.
Tanzania imejipanga kuwapokea na kuwatembeza watalii hao katika vivutio
vya utalii vilivyoko nchini. Serikali inawakaribisha watalii hao
kutembelea vivutio hivyo vya utalii ambavyo nchi imebarikiwa kuwa navyo
ili wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania nchini kwao na
kwingine watakakokwenda.
Imetolewa na:Dkt. Faraji K. Mnyepe

Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DODOMA