Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 wa mawaziri wa mambo ya nje wa afrika, nordic

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Tanzania
inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Nchi za Afrika na Nordic (Norway, Denmark, Finland, Sweden na Iceland)
unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019 kwenye Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. 


Akiongea
na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe
alisema kuwa mkutano huu utafunguliwa rasmi na Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo hii ni
mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2000.  


Kwa
mujibu wa Dkt. Mnyepe, mkutano huu utajumuisha jumla ya mawaziri 34 wa
Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic pamoja na washiriki wengine
ambao idadi yao inatarajiwa kufikia 250. Mawaziri watakaokuja kutoka
nchi za Nordic ni wa nchi za Sweden, Norway, Denmark, Finland na
Iceland. Kutoka nchi za Afrika watakuja Mawaziri wa Algeria, Angola,
Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Comoros na Jamhuri ya Demokrasia
ya Kongo (DRC). 


Nyingine
ni pamoja na Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mali, Malawi,
Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Niger, Rwanda, Senegal, Somalia,
Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, Zambia, Zimbabwe na sisi wenyeji
Tanzania. Aidha, mkutano huo utajumuisha Mawaziri, Mabalozi wa nchi
shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa
nchini pamoja na watendaji wa Serikali. Kauli mbiu ya mkutano huu ni:
“Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu” 


“Mkutano
huu unafanyika hapa Tanzania kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania
na nchi za Nordic ni wa kihistoria na wa kipekee. Ushirikiano huu
ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo Wamisionari kutoka nchi
hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu.
Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole
na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika
Project. Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic
ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu
maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi
wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika,” alisema
Dkt. Mnyepe 


Katibu
Mkuu aliongeza kuwa, “katika nchi za Afrika, Tanzania inapokea misaada
mingi kutoka nchi za Nordic kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa mfano kwa
miaka mitano ya kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, Tanzania imepokea
takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 900 kutoka nchi za Nordic. Nchi
hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu;
afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti;
misitu; usawa wa jinsia; utunzaji wa mazingira; na ukuzaji wa sekta ya
biashara,”. 

“Kufuatia ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi za
Nordic, nchi hizo ziliiomba Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa
mkutano wa mwaka huu kutokana na mahusiano na mazuri yaliyopo na hatua
za kasi za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli, Kutokana na urafiki na historia hiyo hiyo Serikali ya
Tanzania ilikubali kuwa mwenyeji wa mkutano wa mkutano huo na
utafunguliwa na Mheshimiwa Rais. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni,
Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu,” aliongeza Katibu Mkuu  


Aidha,
mkutano huu, utajadili fursa za uwekezaji, biashara, amani na usalama
na masuala mengine mtambuka, kama vile athari za mabadiliko ya
tabianchi. Katika mkutano huu, tutazungumzia pia mahusiano baina yetu na
nchi moja moja hususan ubia wa kimaendeleo. Kutokana na mafanikio
makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya
Tano, wenzetu wa Afrika na Nordic watapenda pia kusikia uzoefu na
mafanikio ya Tanzania kwenye sekta za afya, elimu, nishati, miundombinu,
kilimo, utalii, ukusanyaji wa kodi, mafanikio ya vita dhidi ya rushwa,
ujangili, madawa ya kulevya na maeneo mengine.  


Kwa
upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania, Balozi Elisabeth Jacobsen
alisema kuwa mkutano huu utatoa pia fursa ya mazungumzo ya uwili
(bilateral meetings) kati ya nchi za Nordic na nchi za Afrika. 


“Ni
imani yangu kuwa kupitia mkutano huu tutaweza kujadilili mambo
mbalimbali ikiwemo hatua za kimaendeleo zilizofikiwa katika sekta
mbalimbali hususan afya, huduma za kijamii, elimu na mazingira
kibiashara na uwekezaji kwani Tanzania imekuwa na mahusiano mazuri na
nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Nordic,” alisema Balozi Elisabeth.   


Nae
Balozi wa Sweden nchini, Balozi Anders Sjoberg alisema kuwa mkutano wa
kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001 ambapo baada ya hapo mikutano
kama hii ilikuwa inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la Afrika na
nchi za Nordic.  


“Kwanza
kabisa niipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa Mawaziri
wa Mambo ya Nje, ni fursa kutumia mkutano huu kujadili masuala ya
kibiashara, uwekezaji, amani na usalama kwa maslahi ya nchi za Afrika na
Nordic,” alisema Balozi Sjoberg. 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *