Na Seif Mangwangi
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha
Bara la Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti magonjwa (ECDC) na baadaye ripoti hiyo
kuchambuliwa na kusomwa na kituo kikubwa cha habari cha nchini Ujerumani cha
Deutsche Welle (DW) imeitaja Tanzania kuwa nchi pekee duniani ambayo haijaripoti
maambukizi yoyote ya mgonjwa wa Corona kwa wiki nne (4) zilizopita huku ikiwa
salama na ugonjwa huo hatari duniani kwa sasa kwa takribani wiki 46.
Ripoti hiyo iliyotolewa na kituo
hicho chenye makao makuu yake jijini Solna nchini Sweden, inaeleza kwamba
wakati dunia nzima ikiwa kwenye giza totoro na isijue la kufanya kwa kuendelea
kuripoti maambukizi ya Corona kila kukicha, Tanzania iko salama kabisa na balaa
hilo na watu wakiendelea na shughuli zao za kila siku bila ya vizuizi wala
masharti yoyote ya Corona.
Wakati Tanzania ikitajwa
kutokuwa na virusi vya ugonjwa wa Corona, Nchi nyingi za Afrika zimeendelea
kupokea msaada kutoka China kukabiliana na janga la Corona.
Hivi karibuni China imewasilisha
msaada wa vifaa vya matibabu nchini Uganda na kukabidhi kwa waziri wa afya wa
nchi hiyo Bibi Ruth Aceng.
Balozi wa China nchini Uganda
Bw. Zheng Zhuqiang amesema vifaa hivyo ni pamoja na barakoa za upasuaji elfu
kumi, barakoa za N95 elfu mbili, mavazi ya kujikinga ya kutumia mara moja elfu
mbili, vipimia joto mia tano, miwani ya usalama elfu mbili, glavu za upasuaji
elfu kumi, na kusema shehena ya pili ya msaada huo itawasilishwa hivi karibuni
nchini Uganda.
Bibi. Aceng ameishukuru China
kwa kuendelea kuiunga mkono Uganda haswa katika mapambano dhidi ya virusi vya
Corona.
Wakati huohuo ubalozi wa China
umetoa msaada wa dawa na vifaa vya kupambana na Corona kwa ajili ya watoto wa
Ghana. Waziri wa jinsia, watoto, na ulinzi wa jamii wa Ghana Bibi Cynthia
Morrison ameishukuru China kwa msaada huo.
Msaada kama huo pia umepokelewa
nchini Senegal, ambako waziri wa afya wa Senegal Bw. Abdoulaye Diouf Sarr
ameishukuru China kwa msaada huo na mshikamano inaoonyesha wakati wa mapambano
dhidi ya janga la Corona.
Tanzania kupitia kwa Rais Dkt John
Pombe Magufuli alitoa agizo la misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi kufanyiwa
uchunguzi kabla ya matumizi yake ili kuepuka kupata maambukizi mapya kama
ambavyo imekuwa ikitokea katika nchi nyingi duniani.