- Yaitaka kufanyia mabadiliko sheria ya uchawi kulinda Albino
- Tangu ilipotungwa mwaka 1928 haijawahi kubadilishwa
- Pia yatozwa fidia ya Milioni 10 na kutakiwa kuanzisha mfuko wa fidia kwa watu wenye ualbino
Na Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA ya Afrika ya Watu na Haki za Binaadam (AfCHPR), imeiamuru Serikali ya Tanzania kufanyia mabadiliko sheria ya uchawi ambayo inadaiwa kukosa vifungu madhubuti vinavyoweza kuwatia hatiani watuhumiwa wanaoshtakiwa kwa tuhuma za uchawi.
Aidha mahakama hiyo imeiamuru Serikali ya Tanzania kuanzisha mfuko wa fidia kwa watu wenye ualbino na kwa kuanzia iweke kiasi cha shilingi Milioni kumi (TZS10,000,000/=), fedha ambazo zitatumika kama fidia kwa wote ambao wamekuwa wakikabiliwa na madhila kutokana na ulemavu wao.
Amri hiyo imetolewa leo Februari 5, 2025 chini ya majaji 7 wa Mahakama hiyo kufuatia shauri la madai namba 019/2018 lililofunguliwa na mashirika ya utetezi wa haki za binaadam ikiwemo kituo cha haki za binaadam(CHR),yenye makao yake makuu katika chuo kikuu cha Pretoria nchhini Afrika Kusini, Kituo cha sheria na haki za binaadam Tanzania (LHRC), na Taasisi ya Haki za Kibinadamu na Maendeleo katika Afrika (IHRDA).

Kwa pamoja taasisi hizi zilifungua shauri mahakamani hapo zikidai kuwepo kwa ukiukwaji wa haki kadhaa za watu wenye ualbino ambazo zimekuwa zikilindwa chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Moja ya madai ya walalamikaji katika kesi hiyo ni pamoja na nchi ya Tanzania kukiuka haki watu wenye ualbino chini ya Vifungu 2, 4 5, 7 vya Mkataba na Vifungu 16 na 29 vya Mkataba wa Watoto pamoja na madai ya ukiukwaji wa haki ya kubaguliwa kutokana na ulemavu wao.
Hata hivyo Mahakama hiyo imesema imeweza kuigundua kuwa watu wenye ulemavu wa ualbino wanachukuliwa tofauti hasa kutokana na imani potofu na imani zenye madhara kuhusu nguvu za kichawi zinazohusishwa nao.
“Mahakama pia ilibainisha kuwa ingawa nchi ya Tanzania imechukua baadhi ya hatua za kushughulikia ubaguzi unaofanywa dhidi ya watu wanaoishi na ualbino na kubaini kuwa juhudi hizo zimeshindwa kufikia viwango vya sheria za kimataifa za haki za binadamu, kwa hiyo, Mahakama imeona kuwepo kwa ukiukwaji wa haki ya watu wenye ualbino ya kubaguliwa,”amesema Jaji Stela Anukam alipokuwa akisoma hukumu hiyo leo kwa niaba ya majaji wenzake.
“Pia Mahakama ilizingatia maombi ya Waombaji kwa fidia. Chini ya fidia za Pecuniary, Mahakama iliamuru Nchi inayolalamikiwa ya Tanzania kuanzisha mfuko wa fidia na kulipa katika mfuko huo kiasi cha Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania (TZS 10,000,000) kwa ajili ya chuki ya kimaadili iliyoikumba jamii ya watu wanaoishi na Ualbino ambayo pia itatengeneza fedha za msingi kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa fidia,”amesema Jaji Stella Anukam.
Aidha kuhusu fidia zisizo za kifedha, Mahakama hiyo imeiamuru Nchi ya Tanzania kurekebisha sheria zilizopo ili kuharamisha na kuadhibu vitendo vya unyanyasaji ambavyo vinalenga watu wenye ualbino kuchukulia vitendo kama hivyo kuwa vimefanywa chini ya hali ya hatari.
“Mahakama pia inaiamuri Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ya Uchawi ya mwaka 1928, Sura ya 18 ya Sheria za Tanzania, ili kuweka wazi utata unaohusiana na uchawi na mila na desturi pamoja na kukamilisha, kutangaza na kutekeleza mpango wake wa kitaifa wa uendelezaji na ulinzi wa haki za watu wenye ualbino,”Amesema.
Pia Mahakama hiyo imeiamuru Tanzania kuchukua hatua zote zinazohitajika katika utekelezaji kamili wa haki ya kupata elimu kwa watu wenye ualbino, afya , kuongeza uelewa juu ya imani potofu kuhusu ualbino kwa kufanya kampeni mbali mbali zinazoendelea kwa angalau miaka miwili.
Aidha Serikali ya Tanzania imetakiwa kuandaa na kutekeleza mikakati itakayohakikisha utimilifu kamili wa haki na ustawi wa watoto wenye ualbino, ikiwa ni pamoja na mambo mengine, kulingana na amri ya Mahakama ikiwemo kujumuisha mipango juu ya usalama wao, kisaikolojia, matibabu na usaidizi mwingine muhimu kwa maisha na maendeleo yao.
Mahakama hiyo iliiamuru Serikali ya Tanzania kushirikiana na Waombaji, kuwezesha jitihada za kina na zilizoratibiwa za kupunguza msongamano wa watu katika makazi hayo, kuziunganisha familia na kuhakikisha watoto wenye ualbino katika makazi hayo wanapata huduma za msingi
Shauri hilo lilikuwa likisikilizwa na majaji kumi ambao ni Modibo Sacko, Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Ben Kioko, Jaji Rafaâ Ben Achour, Jaji Suzanne Mengue, Jaji Tujilane R. Chizumila, Jaji Chafika Bensaoula, Jaji Blaise Tchikaya, Jaji Stella I. Anukam, Jaji Dumisa B. Ntsebeza, Jaji Dennis D. Adjei na Msajili wa mahakama hiyo Dkt Robert ENO huku Rais wa Mahakama hiyo Jaji Imani Aboud akiondolewa kutokana na kuwa ni Mtanzania na hivyo kuwa na maslahi na kesi hiyo.

