TASAF kuondoa kaya Laki nne zilizoimarika kiuchumi

Na Seif Mangwangi, APC Media- Arusha

KAYA laki nne (400,000), za wanufaikaji wa ruzuku ya mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ziko mbioni kuondolewa kwenye mpango wa kaya maskini kufuatia kuimarika kiuchumi kiasi cha kuwa na uhakika wa kumudu milo mitatu kwa siku.

Katika taarifa yake kwa Waandishi wa habari na wahariri Jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo Shedrack Mziray, kaya hizo zitaondolewa Septamba mwaka huu baada ya kufanyika kwa tathimini kuhusu wanufaika wa Mfuko huo ambao kwa sasa wanaweza kujimudu kiuchumi.

Wananchi wa Kijiji Cha Songambele wakifuatilia mazungumzo ya Mkurugenzi wa TASAF Shedrack Mziray (hayupo pichani) walipotembelea kituo chaa Afya Songambele kilichojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa TASAF

Mziray amesema Kaya hizo wakati zinaingizwa katika Mfuko huo zilikuwa na hali duni kiuchumi na wengine kutomudu milo mitatu kwa siku pamoja na mahitaji ya msingi ikiwemo kulipia ada Watoto wao.

Amefafanua kutokana na tathimini waliofanya inaonesha kati ya kaya milioni 1,370,000 ambazo zipo katika mpango wa kuwawezesha kiuchumi kutokana na kukabiliwa na umasikini uliokithiri lakini ni kupitia mfuko huo kaya 400,000 zitaondolewa.

“Tunatarajia kuziondoa kaya 400,000 na hii ni baada ya kufanyika tathimini na kubaini sasa wanaweza kujiendesha kiuchumi , baada ya kuwa katika Mfuko wa TASAF na kunufaika na miradi mbalimbali na fedha walizokuwa wakipatiwa hivi sasa wameimarika kiuchumi, mambo yao safi kwani wanajimudu kiuchumi.

Mkurugenzi wa Miradi wa mfuko wa TASAF John Stephen akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa mradi wa TASAF

“Tunafahamu katika kuondoa kaya hizo wakati utakapofika mtasikia malalamiko maana mtu ameshazoea kupewa fedha za TASAF akiambia anaondolewa hawezi kukubali,ingawa wengine wako tayari kwani wanaona kabisa maisha Yao yamekuwa bora ukilinganisha na awali kabla ya kuingizwa TASAF.”

Mziray amesema baada ya kuziondoa kaya hizo watakuwa wamebakiwa na kaya 900,000 ambazo zitaendelea kuhudumiwa na Mfuko huo huku akieleza pamoja na kuondoa kaya 400,000 Kuna kaya nyingine kwa hali ya umasikini walionao hawawezi kutoka leo Wala kesho ingawa kimsingi wanufaika wanatakiwa kufahamu hakuna anayeweza kuhudumiwa na mfuko huo milele.

Hata hivyo amesema kukamilika kwa Awamu ya tatu ya TASAF kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na jitihada za Serikali kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii huku akifafanua mafanikio ya mfuko yametokana na ushirikiano uliopo katika halmashauri mbalimbali ambazo wamekuwa wakitekeleza miradi.

Kuhusu miradi ya maendeleo inayoibuliwa na Wananchi, amesema Mfuko kupitia programu ya kusaidia katika miradi ya maendeleo, amesema kwa Mkoa wa Arusha Kuna miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo miradi katika ekta ya afya, elimu na maji

Amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na watalaamu wa halmashauri ambazo zinatekeleza miradi ya TASAF na kwa sasa halmashauri 186 nchini zinatekeleza miradi ya kimaendeleo.

Mkurugenzi wa TASAF Shedrack Mziray mwenye shuka jekundu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Selemani Msumi wakikagua bweni la wasichana Sekondari ya Oldonyowas lilojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa TASAF