Tbs yafanikisha kusajili majengo zaidi 140 ya chakula na vipodozi mkoani morogoro

 Afisa
Usalama wa Chakula wa TBS Bw. Kaiza Kilango, akikagua majengo ya bidhaa
za chakula na vipodozi katika Halmashauri ya Mlimba mkoani Morogoro
ambapo alibaini uwepo wa bidhaa zilizofika ukomo wa matumizi na
kuziondoa ili ziteketezwe.


Baadhi ya Maafisa wa TBS
wakiwasikiliza wamiliki wa majengo ya biashara ya chakula na vipodozi
katika Halmashauri ya Mlimba, Morogoro ili kuhakikisha wanatoa huduma
katika maeneo safi na salama .




Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
limeendelea na zoezi la kusajili majengo ya chakula na vipodozi katika
Halmashauri za wilaya ya Mlimba na Ulanga mkoani Morogoro ambapo zaidi
ya majengo 140 yamesajiliwa katika maeneo hayo.


Usajili huu wa majengo ya chakula
na vipodozi unaenda sambamba na ukaguzi bidhaa katika majengo na maduka
pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo
Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Bw. Daniel Kahabi amesema Shirika
limejikita katika kuhakikisha linafika katika pande zote za nchi na
kufanya usajili wa majengo hayo sambamba na kutoa elimu ya namna bora ya
uhifadhi wa bidhaa pamoja na kuhakikisha majengo yao yamekidhi vigezo
vinavyohitajika.


“Sambamba na usajili na ukaguzi wa
majengo na bidhaa za chakula na vipodozi, tunawasihi wenye maduka
wanakagua mara kwa mara bidhaa zao ili kuhakikisha wanauza bidhaa ambazo
hazijakwisha muda wa matumizi lakini pia wahifadhi vizuri bidhaa zao
sehemu ambazo ni safi na salama” alisema Bw. Kahabi.


Kwa upande wake Afisa Masoko wa
TBS Bi. Deborah Haule ametoa wito kwa wafanyabiashara wa chakula na
majengo kusajili majengo yao katika mfumo ili kuepuka usumbufu wanaoweza
kuupata pindi wakaguzi watakapopita katika maeneo yao.


“Usajili unafanyika kwa njia ya
kielektroniki ukiingia katika tovuti ya TBS na kwenda katika huduma
mtandao unaweza kujisajili wakati wowote na mahali popote, unatakiwa
kuwa na TIN pamoja na leseni ya biashara ili kukamilisha usajili “.
Alisema Bi. Deborah.


Majukumu haya ya usajili wa
majengo ya chakula na vipodozi yalikasimishwa rasmi kwa TBS Juni 2019
ambapo hapo awali yalikua yakifanywa na iliyokuwa na TFDA.