Tbs yaokoa takribani bilioni 2.7 katika zoezi la ukaguzi wa magari

 

 

Waziri wa Viwanda na Biashara
Prof.Kitila Mkumbo (katikati) akizungumza na watumishi wa TBS ambao
wanahusika na ukaguzi wa magari bandarini mara baada ya kutembelea
bandari katika kitengo cha kukagua magari zoezi ambalo linafanywa na TBS
na kujiona shughuli hiyo ikifanyika.


  1. Waziri wa Viwanda na Biashara
    Prof.Kitila Mkumbo akiangalia namna zoezi la ukaguzi wa magari bandarini
    unafanyika baada ya kutembelea bandari katika kitengo cha kukagua
    magari zoezi ambalo linafanywa na TBS na kujionea shughuli hiyo
    ikifanyika.


Waziri wa Viwanda na Biashara
Prof.Kitila Mkumbo akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Dkt.Athuman Ngenya mara baada kutembelea bandarini
katika kitengo cha kukagua magari zoezi ambalo linafanywa na TBS na
kujionea shughuli hiyo ikifanyika.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Dkt.Athuman Ngenya akizungumza mbele ya Waziri
wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo mara baada ya Waziri huyo
kutembelea bandarini katika kitengo cha kukagua magari zoezi ambalo
linafanywa na TBS na kujionea shughuli hiyo ikifanyika.


Meneja wa Ukaguzi wa Bidhaa
zinazotoka nje TBS, Mhandisi Saidi Mkwawa akizungumza mbele ya Waziri wa
Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo mara baada ya Waziri huyo
kutembelea bandarini katika kitengo cha kukagua magari zoezi ambalo
linafanywa na TBS na kujionea shughuli hiyo ikifanyika.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)


******************************


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM


Katika kipindi cha mwezi Aprili
hadi kufikia Agosti 3, 2021 Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limekusanya takribani Shilingi Bilioni 3.9 katika zoezi la ukaguzi wa
magari bandarini yanayotoka nje ya nchi na kuokoa kiasi cha shilingi
Bilioni 2.7 ambayo mwanzo ilikuwa inabaki nje kabla ya zoezi hilo kuanza
kufanyika hapa nchini.


Ameyasema hayo leo Waziri wa
Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo mara baada ya kutembelea bandari
katika kitengo cha kukagua magari zoezi ambalo linafanywa na TBS na
kujionea shughuli hiyo ikifanyika.


Amesema mpaka kufikia Agosti 3,
2021 TBS ilifanikiwa kukagua magari 11079 na katika magari hayo 7700
yalikuwa yamekidhi ubora na magari yaliyobaki yalikwenda kutengenezwa na
baada ya kutengenezwa magari 1890 yaliweza kukidhi ubora na mengine
yaliyobaki yapo gereji yakiendelea kurekebishwa.


“Kwa kuamua kutekeleza mpango huu,
Serikali inaokoa fedha nyingi ambazo zingebaki nje hivyo kwa kipindi cha
miezi mitatu tumekusanya takribani Bilioni 3.9 na fedha hii inaingia
katika mfuko mkuu wa Serikali”. Amesema Prof.Mkumbo.


Aidha Prof.Mkumbo ametoa wito kwa
waingizaji wa magari nje ya nchi kushirikiana ipasavyo na TBS ili zoezi
liweze kwenda vizuri hasa kuendelea kuelezea changamoto ambazo zimekuwa
zikijitokeza ili waweze kuzitatua.


Pamoja na hayo Prof.Mkumbo ameipongeza TBS kwa juhudi ambazo wanazifanya katika mpango wa ukaguzi wa magari bandarini.


Kwa upande wake Meneja wa Ukaguzi
wa Bidhaa zinazotoka nje TBS, Mhandisi Saidi Mkwawa amesema kuna magari
1890 hayakufaulu kwenye hatua ya awali yanahitaji marekebisho ya taa,
matairi na mengineyo, na hili lote limekuwa likiwanufaisha Watanzania
kwasababu yanakwenda katika gereji ambazo Watanzania wanazimiliki .


“Bado dhamira yetu na jukumu letu
la kukuza biashara inafanyika na tumeamua kufanya kazi hii kwa weledi
lakini kikubwa kituo hiki kuanzia wiki ijayo tunaanza kujenga kituo
kikubwa Cha kudumu ambacho kitakuwa na uwezo wa kupima vitu vingi na
kukagua magari mengi”. Amesema Mhandisi Mkwawa.


Katika utaratibu wa zamani ambapo
ukaguzi wa magari kwa kiasi kikubwa ulikuwa unafanyika nje ya nchi na
TBS kwa niaba ya Serikali tungepata asilimia 30% tu za fedha peke yake
na asilimia 70% ingebaki nje.