Tbs yatoa mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani morogoro

 


Wakaguzi wa TBS wakielimisha baadhi ya wauzaji wa maduka ya chakula mkoani Morogoro, namna ya kusajili katika mfumo na umuhimu wa kutumia vifungashio sahihi katika bidhaa zao.

Wakaguzi
wa TBS wakielimisha baadhi ya wauzaji wa maduka ya chakula mkoani
Morogoro, namna ya kusajili katika mfumo na umuhimu wa kutumia
vifungashio sahihi katika bidhaa zao.

Washiriki wa mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani Morogoro wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo.

Washiriki wa mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani Morogoro wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limeendelea kutoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali na wafanyabiashara
kwa ujumla wanaojishughulisha na sekta ya mafuta ya kula 282 kutoka
katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero na Halmashauri ya Mji ya Gairo za mkoani Morogoro.

Mafunzo haya maalum yamewalenga
wajasiriamali na wafanyabiashara wanaojishughulisha na uzalishaji,
usambazaji na uuzaji wa mafuta ya kula katika masoko ya ndani na ya nje
katika mkoa wa Morogoro.

Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS
Dkt. Athuman Y. Ngenya, Meneja wa Utafiti na Mafunzo wa TBS Bw. Hamisi
Mwanasala alisema mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya
Shirika sambamba na agizo la Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na
Biashara kulitaka Shirika kuendesha mafunzo haya maaalum mikoa yote
nchini.

Bw. Sudi alisema Serikali inatambua na
kuthamini mchango wa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na wanaojishughulisha
na sekta mafuta ya kula katika kukuza uchumi wa nchi.Hivyo mafunzo haya
ni mahsusi kuwajengea uwezo wadau wa mafuta ya kula nchini ili waweze
kuzalisha mafuta kwa wingi na yenye ubora unaokidhi matakwa ya viwango
vya mafuta ya kula.

“Mafunzo haya yataenda sambamba na utoaji
wa elimu maeneo ya kwenye masoko na vituo vya pembezoni mwa barabara
ambapo wauzaji wengi wanauza mafuta ya kula” alisisitiza Bw. Sudi.

Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora wa
TBS, Bi Gudila Boniface alisema ili mafuta ya kula yakidhi viwango ni
lazima kufuata kanuni za kilimo bora, usindikaji na usafi.

Bi. Gudila alisema kanuni za kilimo bora zinahusisha matumizi ya mbegu bora, kuvuna kwa wakati mazao yalikomaa.

Kwa upande wa kanuni bora za usindikaji
kwa mujibu wa Bi. Gudila ni pamoja na kutumia malighafi bora, vifaa vya
kusindikia ambavyo havishiki kutu na vilivyoshauriwa na wataalam.

Akizungumzia kanuni bora za usafi, Bi.
Gudila alisema wazalishaji wanatakiwa kuhakikisha vifaa vya kuhifadhi
mafuta ni safi ikiwa ni pamoja na madumu yanayotumika kuhifadhi mafuta
hayo yawe yamesafishwa vizuri pamoja na usafi wa mazingira.

” Vifungashio/Madumu wanayoweka mafuta
wahakikishe wameyasafisha vizuri na waweke lebo zinazoeleza bidhaa hizo
ni za aina gani,” alisema na kuongeza kwamba haikubaliki kwenye
vifungashio ambavyo wazalishaji wanaweka mafuta iwe lebo inayohusu
bidhaa nyingine.

Aidha, alisema mafuta ya kula hayatakiwi
kuwekwa juani, kwani yanapokuwa juani kuna kemikali zinazozalishwa na
zinaweza kusababisha mafuta kuharibika ambayo yakitumiwa na walaji
yanaleta athari za kiafya.

Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora
Mwandamizi wa TBS, Bi. Flora Luvanda alitoa wito kwa wadau hao
kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, kusajili bidhaa za chakula na vipodozi
na majengo yanayojihusisha na bidhaa za vyakula na vipodozi.

” Tunatoa wito kwa wadau kuwasiliana na
TBS endapo wanakutana na changamoto yeyote wakati wa usajili
tutawaelekeza na kuwasaidia mpaka usajili utakapokamilika,” alisema Bi
Flora.

Alisema ni muhimu kwa wafanyabishara
kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria
ambayo imetokana na mabadiliko ya Sheria ya fedha ya mwaka 2019
iliyohamisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na
vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokua Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania
(TFDA).

Alisema usajili wa bidhaa na majengo ya
vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria na hivyo kwa kufanya hivyo
kutawafanya wafanye biashara zao kwa uhuru na uhakika.

Katika mafunzo haya, TBS imewashirikisha
watoa mada kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi nyingine
ikiwa ni pamoja na Wakala wa Vipimo (WMA), BRELA, Shirika la Kuhudumia
Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na maafisa kutoka dawati la Halmashauri
husika ikijumuisha Afisa Biashara, Afisa Afya na Afisa Maendeleo ya
Jamii.

Mafunzo haya maalum kwa wadau wa mafuta
ya kula mkoani Morogoro ni mwendelezo wa mafunzo kama haya yaliyokwisha
kutolewa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Iringa,
Njombe, Mbeya na Songwe.