Ttra yang’ara tuzo za nbaa , yapata ushindi wa jumla

Na Veronica Kazimoto-Dar es Salaam

Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imeshinda tuzo mbili ikiwemo mshindi wa jumla
katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu mwaka 2018 kwa kufuata viwango
vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Taasisi za Umma yaani mfumo
wa IPSASs.


Katika
hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
NBAA Bunju jijini Dar es Salaam, TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika
uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwenye kipengele cha Wakala wa
Serikali na mshindi wa jumla kwa taasisi, wakala, kampuni na mashirika
mbalimbali ambayo yamefanya vizuri katika kuandaa taarifa za fedha
katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza
mara baada ya kupokea tuzo hizo, Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Edwin Mhede,
ameipongeza Idara ya Fedha na idara nyingine ndani ya mamlaka hiyo kwa
kufanikisha upatikanaji wa tuzo hizo.

“Nachukua
nafasi hii kumshukuru mkuu wa idara anayehusika na Idara ya Fedha
pamoja na wakuu wa idara nyingine ndani ya mamlaka maana zote zinatoa
mchango mkubwa kuhakikisha idara hii inatoa taarifa sahihi na zenye
kuleta mipango sahihi kwa mamlaka na serikali kwa ujumla,” alisema Dkt.
Mhede.

Dkt.
Mhede alieleza kuwa, taarifa sahihi ni msingi wa mipango kwa kuwa
taasisi isiyopanga kushinda ni sawa na taasisi inayopanga kushindwa
hivyo suala la uandaaji bora wa taarifa za hesabu ni moja ya ufanisi wa
ofisi yoyote hapa ulimwenguni.

Bodi
ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) ndio hutoa tuzo hizo kila mwaka
ambapo mwaka 2017 TRA iliibuka mshindi wa kwanza tena katika uandaaji
bora wa taarifa za hesabu katika kipengele cha Wakala wa Serikali.