Tucta yasema kuna ongezeko kubwa la wafanyakazi kuomba kustaafu kwa hiari


Na Amiri Kilagalila-Njombe

Rais
wa shirikisho la vyama vya wafanya kazi Tanzania TUCTA ambaye pia ni
makamu mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania
TALGWU bw.Tumaini Nyamhokya,amesema ni haki ya mfanyakazi kustaafu kwa
hiari hivyo shirikisho halina tamko kwa wafanya kazi kutokana na habari
zilizoenea mitandaoni kuwa watumishi wengi wameanza kuomba kustaafu kwa
kuhofia KIKOKOTOO.
Rais wa TUCTA ameyasema hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa chama cha
wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU mkoa wa Njombe ambao
hufanyika kila baada ya miaka miwili ukiambatana na uchaguzi wa viongozi
wa chama hicho.


“Nimeulizwa na waandishi wa habari wengi kwamba watumishi wanastaafu kwa
hiari wanakuwa na hofu,kustaafu kwa hiari kupo kwa mujibu wa sheria,mtu
akiona atumie kustaafu kwa hiari ili apate fedha afanye mambo yake
mengine hilo ni jambo jingine,na kama kuna mtu ameamua kustaafu kwa
hiari ili asifike kule ambako kuna sintofahamu kwamba kuna KIKOKOTOO
gani kitafuatia hiyo pia ni haki yake kwa mujibu wa sheria”alisema
Nyamhokya


Nyamhokya ameongeza kuwa shirikisho hilo halina tamko la kuwaondoa hofu wafanyakazi.


“Kwa hiyo sisi hatuna tamko lolote la kuwaambia wafanyakazi,hatuna tamko
lolote la kuwaondoa hofu,hofu ilikuwepo kubwa sana wakati kikokotoo
kimebadilika na kikaja  kikokotoo ambacho kiukweli tunakiita kikokotoo
kandamizi katika masalahi ya wafanyakazi hasa wale ambao wamekuwa
wamestaafu sasa tumerejeshewa kiu na tumepewa muda wa miaka mitano
tuweze kusimamia na kuandaa kwa hiyo timu zipo na zinaendelea kufanya
kazi kuhakikisha tunaandaa kikokotoo ambacho kitakuwa rafiki kwa pande
zote Mbili”aliongeza Nyamhokya


Katika hatua nyingine Nyamhokya amesema bado kuna badhi ya viongozi wa
serikali na wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya kazi za kimihemko na
kuwaumiza watendaji hali ambayo inasababisha kuvunjika moyo kiutendaji.


“Sehemu kubwa viongozi wanakwenda vizuri lakini kuna baadhi ya wanasiasa
ambao ni wateule wa mheshimiwa Rais, sisi kama viongozi wa vyama
tunaona hawatendi vyema,baadhi tumeona wana hulka ya kuchukua hatua
zinaonekana kuwa za kinidhamu kwenye majukwaa,utaona wanatamka simtaki
mtumishi huyu mkoani kwangu,au wanasema kuanzia sasa wewe sio mkuu wa
idara kiukweli inaumiza sana”alisema Nyamhokya


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *