Tume ya haki za binaadam na utawala bora tanzania yatoa pongeza kwa rais magufuli kwa kutoa msamaha kwa wafungwa 5000


Itakumbukwa kuwa Desemba, 9, 2019 katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Uhuru, Mheshimiwa Rais John Magufuli alitangaza msamaha na kuwaachia huru wafungwa 5,533.

Uamuzi huo wa Rais wa kuwasamehe wafungwa alioutoa wakati akihutubia wananchi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza umekuwa ukitekelezwa na wakuu wa nchi tangu tupate uhuru mwaka 1961.
 Hata hivyo, uamuzi wa Rais kuwasamehe wafungwa 5533 ni wa kipekee tangu Tanzania ipate uhuru kutokana na idadi kubwa ya wafungwa aliowasehe.

Kufuatia uamuzi huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake huo uliojaa upendo kwa wananchi anaowaongoza.

Tume inachukulia uamuzi huo wa Rais kama jambo ambalo linaweka nguvu na mkazo katika sehemu ya majukumu yake ya kuhakikisha haki za binadamu zinafurahiwa na watu wote ikiwemo wale walio magerezani.
Aidha, Tume imefurahishwa na kauli aliyoitoa Mhe. Rais katika maadhimisho hayo kuhusu kusikitishwa kwake na hali ya magereza, kwani kauli hiyo inaonesha dhamira ya dhati aliyonayo yeye binafsi na serikali yake katika kulinda na kuhifadhi haki za Wafungwa na Mahabusu katika magereza hapa nchini.

Moja ya Jukumu la Tume kwa mujibu wa ibara 130 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 6 (1) cha sheria ya Tume ni kutembelea magereza ili kuangalia uhifadhi wa haki za binadamu katika sehemu hizo na kutoa mapendekezo yanayofaa katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya magereza yetu.

Tume imekuwa ikifanya ziara za mara kwa mara katika Magereza mbali mbali kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo. Katika ziara zake Tume imekuwa ikigundua changamoto kadhaa zinazowakabili wafungwa na mahabusu zikiwemo mlundikano wa wafungwa na mahabusu, na kesi zao kuchukua muda mrefu kumalizika. Tume imekuwa ikitoa mapendekezo kwa taasisi husika kurekebisha hali hiyo.
Kwa kauli hiyo ya Mhe. Rais, Tume inaamini kuwa taasisi zenye dhamana ya kuhifadhi wafungwa na mahabusu wataongeza kasi katika kulinda na kuhifadhi haki za makundi hayo.
Tume inaamini pia, kauli hiyo itazifanya taasisi zenye dhamana ya upelelezi kufanya kazi hiyo kwa haraka ili kupunguza muda wa mahabusu kukaa magerezani kwa muda mrefu.
Kwa upande mwingine Mahakama na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka  hazina budi kuongeza juhudi katika kusikiliza na kumaliza kesi za jinai kwa haraka ili kupunguza muda wa mahabusu kukaa magerezani .
Tume inaziomba taasisi zote zenye dhamana ya usimamizi wa jinai kuichukulia kauli hiyo kama ni chachu katika utekelezaji wa majukumu yao hasa ya kulinda na kuhifadhi haki za wafungwa na mahabusu magerezani.

Mwisho, Tume inatoa ushauri kwa jamii na wanufaika wa msamaha wa Mhe. Rais kama ifuatavyo; 1. Wafungwa wote walionufaika na msamaha huo, watumie mafunzo waliyoyapata wakiwa gerezani kushirikiana na Watanzania wenzao kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda.

2. Wanufaika wa msamaha huo wakayatumie vyema mafunzo na maarifa waliyoyapata kufanya kazi za uzalishaji mali na kujipatia kipato; kwani tume inaamini wakifanya hivyo ndio njia pekee ya kumpa faraja Mhe. Rais kwa uamuzi wake.

3. Tume inawasihi Watanzania wote kuwapokea ndugu zao hawa kwa mtazamo chanya na kushirikiana nao katika kazi za ujenzi wa taifa, kwani kinyume na hapo, wakiwatenga itawajengea picha ya kuona wananyanyapaliwa na hivyo kupelekea uwezekano wa kurudia makosa yatakayowarudisha tena gerezani.